Friday, 13 October 2017

Viongozi wa Makundi ya What's App Sasa Kitanzini

Jeshi la polisi kitengo cha makosa cha makosa ya mtandaoni limewatahadharisha viongozi wa makundi ya What's App na kuwataka kutoa taarifa pindi uhalifu unapofanyika kwenye makundi yao.

Kufanya hivyo kutasaidia polisi kuchukua hatua dhidi ya mhusika aliyefanya uhalifu huo ili kukabiliana na ongezeko la vitendo vya uhalifu mtandaoni.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa na naibu mkuu wa kitendo hicho, Joshua Mwangasa wakati wa semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano(TCRA) na kuwakutanisha viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema makosa ya kimtandao yameendelea kuongezeka kwa kasi kubwa huku makundi ya What's App yakionekana kuwa kichocheo kikubwa.

Mwangasa amesema viongozi wa makundi hayo hawatakiwi kuvumilia makosa hayo hivyo wanatakiwa watoe taarifa polisi.

"Usikubali umeanzisha kundi kwa nia nyingine halafu mtu au watu wanaweka mambo yasiyofaa, toa taarifa hatua zichukuliwe kinyume na hapo hata wewe utahusika,"

Amesema kwa kiasi kikubwa makundi hayo yamekuwa yakitumika kusambaza taarifa za uongo na uchochezi.

Mwangasa ametumia fursa hiyo kuwaomba  viongozi wa dini kuwahubiria waumini wao juu ya matumizi sahihi ya mitandao ili kujiweka mbali na uhalifu.

"Ukosefu wa maadili ndio unachangia haya yote haya, ndiyo sababu narudi kwenu viongozi wa dini wasisitizeni waumini wenu watumie mitandao kwa maendeleo," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema mamlaka hiyo inaendelea kuchukua hatua kuimarisha ulinzi wa mawasiliano mtandaoni.

Amesema simu za mkononi kwa sasa zimekuwa kama silaha hivyo matumizi yake yanapaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi. 

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search