Monday, 9 October 2017

Waioteuliwa na Rais Waeleza Namna Walivyopata Taarifa za Uteuzi Wao

Waioteuliwa na Rais Waeleza Namna  Walivyopata Taarifa za Uteuzi Wao
Wakati mawaziri na manaibu walioteuliwa wakitarajiwa kuapishwa leo, baadhi wameeleza namna walivyopokea taarifa za uteuzi wao.

Lakini walioachwa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa juzi na Rais John Magufuli, wamekataa kuzungumzia lolote kuhusu uamuzi huo.

Baadhi ya walioteuliwa wameonyesha dhahiri kutokuwa na taarifa za awali kuhusu uteuzi wao, wengi wakisema walikuwa wakiendelea na shughuli nyingine za kichama na kitaifa.

“Nimepokea uteuzi nikiwa kazini kwenye kikao cha Kamati ya Utekelezaji UWT (Umoja wa Wanawake wa CCM) wa Mkoa Pwani,” ameandika Subira Mgalu katika ukurasa wake wa Facebook.

“Nimetoa machozi kwa imani kubwa aliyoionyesha Mhe Rais Dk John Pombe Magufuli kwangu ni kubwa. Sikutarajia! Ahsante sana Mhe Rais.”

Mgalu, ambaye amekuwa naibu waziri wa Nishati, ametuma picha zinazomuonyesha akiwa na wanachama wengine wa CCM wanaoshangilia, huku akionekana kufuta uso, mithili ya mtu anayefuta machozi.

“Ahsanteni wote. Mlionipongeza wengi sana, nimeona upendo wenu kwangu. Kikubwa mniombee kwa imani zenu tofauti.

“Ahsante wanawake wa Mkoa wa Pwani kwa kuniamini na leo kunisaidia kuhimili jambo kubwa kama hili. Namuomba Mwenyezi Mungu aniongoze vyema katika majukumu haya Amin.”

Hali ilikuwa kama hiyo kwa Dk Hamisi Kigwangalla, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Afya na sasa anakuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Katika akaunti yake ya Instagram, Dk Kigwangalla amesema alipata taarifa akiwa Kituo cha Afya cha Kilimarondo wilayani Nachingwea mkoani Lindi.

“Baada ya kumaliza kazi kituoni hapo na kuanza ku-rake (kusafisha) njia ya kuelekea Liwale, Kituo cha Afya cha Kibutuka, ndipo mwenyeji wetu anaarifiwa na watu wa Liwale kuwa itakuwaje? Mheshimiwa ataendelea na ziara huku amebadilishiwa majukumu?” ameandika Dk Kigwangalla katika mtandao wa kijamii.

“Kilimarondo hakuna mtandao zaidi ya TTCL. Ni kilomita takriban 100 za vumbi kuelekea ndani huko. Ni tarafa ya pembezoni kwelikweli. Ni mahali ambapo Nachingwea inapakana na Tunduru.

“Namba za NW AMJW (Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto) ilibidi ziondolewe na safari ya kutoka huko ianze! Nimepokea salamu nyingi za pongezi na shukrani kwa Mungu aliye juu. Sitaweza kumjibu kila mtu. Uungwana ni kutambua pongezi zenu na dua tele mlizotuombea, nawashukuru sana ndugu zangu. Tuzidi kuombeana dua tu.”

Lakini hakuchelewa kuonyesha ugumu wa kazi iliyo mbele yake.

“Tuna kazi ngumu ya kukimbia kukidhi matarajio ya kiongozi mkuu aliyetuamini na matarajio ya wananchi,” ameandika.

“Binafsi nawaahidi nyote kuwa sitawaangusha! Ahsanteni sana ndugu zangu, natarajia ushirikiano wenu wa kila hali,” alisema.

Mwingine ni Mary Mwanjelwa, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo. Hata hivyo, hakuwa amejiandaa kuzungumzia suala hilo wakati mwandishi wetu alipowasiliana naye kwa simu.

“Kwa sasa nipo Uwanja wa Ndege wa Songwe najiandaa kuruka kwenda Dar es Salaam. Hivyo siwezi kuzungumza chochote kwa sasa. Lakini ni maombi yenu na naomba tuendelee kuombeana,” alisema Mwanjelwa, ambaye aliwahi kushika uenyekiti wa Bunge kwa muda mfupi.

Mteule mwingine ambaye anakuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga alimshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini.

“Nashukuru Rais kwa kuniteua ili nimsaidie katika wizara ambayo ina changamoto nyingi. Naahidi kufanya kazi kwa weledi ili kukabiliana na changamoto zilizopo,” alisema.

Shukrani pia zilitolewa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe, ambaye alisema yuko tayari kufanya kazi kama ambavyo Rais Magufuli alivyomteua.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye alisema, “Nimepokea uteuzi kwa mikono miwili sitamwangusha Rais”.

Aliahidi kufanya kazi ili kusukuma mbele maendeleo ya Taifa.

“Niko njiani kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuapishwa,” alisema Nditiye ambaye ni mbunge wa Muhambwe mkoani Kigoma.

Wakataa kuzungumza

Hali ilikuwa tofauti kwa walioachwa katika mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri.

“Sina cha kusema,” alisema aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani.

Jibu kama hilo lilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe aliyesema hawezi kuzungumzia kuondolewa kwake katika nafasi ya uwaziri.

“Naomba leo nisizungumze chochote please (tafadhali) niacheni kwa sasa,” alisema.

Wizara hiyo imekuwa kaa la moto kwa wanaoteuliwa kuiongoza kutokana na kuwapo mabadiliko ya mara kwa mara.

Mbali ya hao, aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alikataa kuzungumzia suala hilo.

“Sasa unataka nizungumze nini, sina cha kuzungumza,” alisema na kukata simu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search