Friday, 6 October 2017

WALIOFARIKI KWA KUNYWA GONGO DAR WAFIKIA 10

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema idadi ya watu waliofariki dunia kwa kunywa kinywaji kinachosadikiwa kuwa gongo imefikia 10.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema leo Alhamis kuwa wananchi walitoa taarifa baada ya hali za waliotumia pombe hiyo eneo la Kimara kubadilika.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Mohamed Issa (67), Kabugi Rashid (64), Stanslaus Joseph (58), Stephen Isaya (61), Monika Rugaillukamu (42), Alex Madega (41), Hamis Mbala (35) na Ekson Nyoni (28).

Wengine ni mwanamke aliyekuwa akiuza pombe hiyo aliyefahamika kwa jina moja la Anoza na Maleo Ramadhan (45) mkazi wa Kimara Stop Over.

Kamanda Mambosasa amesema katika upelelezi wa awali wamebaini chupa tatu za ujazo wa lita moja zikiwa zimejazwa pombe inayodhaniwa kuwa ni gongo.

"Vielelezo vyote vya tukio hili vimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo," amesema.

Amesema upelelezi unaendelea kubaini wote waliohusika katika tukio hilo, akiwataka wananchi kuacha kunywa na kula vitu visivyo na ubora wala kuhakikiwa na mamlaka husika.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search