Thursday, 9 November 2017

FAMILIA YA TUNDU LISSU YALITAKA BUNGE KUTOKUKWEPA WAJIBU WAKE JUU YA MATIBABU YA NDUGU YAO

Familia ya Tundu Lissu Yataka Bunge Kutokwepa Matibabu ya Ndugu Yao
Familia ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu imeibuka kwa mara nyingine ikiliomba Bunge kutokukwepa wajibu wa kugharimia matibabu ya ndugu yao kwa kuwa si hisani bali ni stahiki anazopaswa kupewa.

Pia, familia hiyo imesisitiza wito wake kwa Serikali wa kuruhusu uchunguzi kutoka nje ili ukweli ujulikane kuhusu waliohusika kumjeruhi kwa risasi Lissu Septemba 7, mjini Dodoma.

Imesema haiwezekani miezi miwili imepita tangu aliposhambuliwa lakini hakuna taarifa za kukamatwa kwa mtu yeyote.

Vincent Mughwai, ambaye ni mdogo wa Lissu alisema hayo jana katika ofisi za Mwananchi, Tabata- Relini jijini Dar es Salaam.

Kwa mwezi wa pili sasa Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

“Miezi miwili imepita gharama za matibabu ziko juu na ni wananchi wa Tanzania ndiyo wamezilipa. Mshangao wetu ni kuwa, Lissu ni mbunge na kama kiongozi ana haki ya kutibiwa na si kubaguliwa,” alisema Mughwai.

Alisema, “Lissu ana bima, bado hajaweza kupata msaada na sisi tunasema kulikoni, kama viongozi wengine wakiugua gharama zao zinalipwa na Bunge, huyu pia ni mbunge kwa nini kunakuwa na double standard kwa ndugu yetu.”

Mughwai alisema kikao walichokaa na uongozi wa Bunge, Oktoba 2 kujadili matibabu kilikwenda vizuri na wao kama familia walieleza kutokuwa na pingamizi la ndugu yao kugharamiwa lakini tangu siku hiyo mpaka sasa hakuna taarifa zozote kutoka kwa Bunge.

“Familia hatujajulishwa ingawa tuliandika si barua bali ujumbe kwamba familia haina tatizo Bunge kulipa gharama za matibabu ya Lissu lakini kimya, Bunge wanajua huyu mgonjwa anaishije huko? Tunaomba apate stahiki zake kama anavyostahili,” alisema.

Kauli hiyo ililifanya Mwananchi kumtafuta Spika wa Bunge, Job Ndugai lakini hakuweza kupatikana huku Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai akisema ‘’mimi sijui na sijapata taarifa kuhusu suala hilo kwani mazungumzo yalipofanyika mimi sikuwapo.”

Mdogo huyo wa Lissu alisema ‘’sisi tunaendelea kuwashukuru Watanzania kwa kujitoa, Chadema kikiongozwa na Mbowe (Freeman Mbowe-Mwenyekiti wa Chadema) ambao mpaka sasa wapo Nairobi, hatuna cha kuwalipa, tunaomba muendelee kumwombea na kutoa michango kupitia akauti za Chadema ili ndugu yetu aweze kupona.”

Kuhusu uchunguzi, Vicent alisema, “Tunaendelea kusisitiza Serikali iruhusu uchunguzi kutoka nje, waje washirikiane na jeshi letu la polisi, huu uvumi kwamba anayehusika ni fulani utamalizika, kama ni Chadema wamehusika watajukikana, kama ni nani watajulikanani hofu iko wapi,” alihoji Vicent

Alitolea mfano, Meja Jenerali mstaafu Vicent Mribata aliyepigwa risasi maeneo ya Ununio- Tegeta jijini humo kuna watuhumiwa walikamatwa lakini tukio la Lissu mpaka sasa hakun taarifa zaidi ya magari kumi aina ya Nissan kukamatwa nayo haijulikani yalipo.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limekuwa likieleza kwamba uchunguzi wa suala hilo unaendelea na hauwezi kuwekwa hadharani kila hatua na mara baada ya kukamilika wataueleza umma

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search