Thursday, 23 November 2017

HOSPITALI YA TAIFA KUOKOA MABILION TIBA YA INNI

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, imeanza kutekeleza mpango wa mwaka mmoja wa kuandaa watalamu kwa ajili huduma ya upasuaji na upandikizaji ini.

Kwa mujibu wa taarifa ya MNH, hospitali hiyo kuu ya rufaa nchini, itakuwa ya kwanza kutoa huduma hiyo katika Afrika Mashariki.

MNH inaandaa wataalamu kwa ajili ya upasuaji ili kuondoa uvimbe ndani ya ini.

Wataalamu hao pia wataandikiza ini, na watatibu homa ya ini ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na magonjwa sanjari na kupunguza rufaa zilizokuwa zinahitajika kwenda nje ya nchi.

Kwa sasa gharama ya tiba ya upasuaji na upandikizaji kwa mgonjwa wa ini lililodhurika au kushindwa kufanya kazi, inafikia wastani wa Sh milioni 100 za Tanzania. 

Wataalamu saba wa MNH wakiwemo madaktari na wauguzi, mwezi huu wanatarajiwa kwenda India kujifunza tiba ya ini.

Kwa mujibu wa daktari bingwa magonjwa ya tumbo na ini katika Idara ya Tiba hospitalini hapo, Dk John Rwegasha, ndani ya mwaka kuanzia sasa huduma ya uchunguzi wa mfumo wa ini na upasuaji mkubwa wa ini, itakuwa imeanza hospitalini hapo.

Dk Rwegasha alisema hayo alipozungumza na HabariLeo kuhusu jitihada wanazozifanya kupunguza vifo na rufaa za kwenda nje ya nchi kutibiwa ini.

 Kwa mujibu wa Dk Rwegasha, huduma hiyo itakapoanza MNH, hospitali itakuwa ikiongoza kutoa huduma hiyo ya kibingwa miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa madaktari wa ndani ya nchi na nchi za EAC hasa Uganda kwa lengo la kutimiza azma, kuwawezesha watalaamu kumudu huduma za tiba za awali kwenye eneo hilo.

Dk Rwegasha alisema kabla ya kuboreshwa kwa kitengo cha mfumo wa chakula na ini mwaka 2014, walikuwa wakitibu wagonjwa wachache wenye matatizo ya vidonda vya tumbo, lakini sasa wanatibu matatizo mengi ya aina mbalimbali ya mfumo wa chakula na ini, yakiwemo ya saratani za koromeo la chakula, uvimbe katika utumbo, kongosho, mfumo wa ini na nyongo kama kutoa mawe na kuzibua uvimbe kwenye mifereji ya ini.

Kwa mujibu wa daktari huyo, pia wanazuia utapikaji damu unaotokana na kusinyaa kwa ini, kunakochangia kupoteza damu nyingi na kupoteza maisha kirahisi. 

Hivi karibuni kitengo hicho kilianza kutibu wagonjwa wa homa ya ini na kufikia sasa wastani wa wagonjwa 1,000 ndani ya mwaka mmoja wamefanyiwa uchunguzi wa homa ya ini na tayari wagonjwa 100 wanapatiwa huduma bure ya tiba homa ya ini kupitia ufadhili wa shirika la CDC.

IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI - HABARILEO

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search