Monday, 27 November 2017

LIPUMBA:SIKUTARAJIA KAMA SLAA ANGEKUWA BALOZI

Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amezungumzia uteuzi wa Dk Wilbroad Slaa kuwa balozi akisema hakutarajia.

Rais John Magufuli juzi alimteua Dk Slaa aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema kabla ya kukihama chama hicho wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wakati wa mchakato wa uchaguzi huo, Profesa Lipumba na Dk Slaa ambao vyama vyao vilikuwa katika umoja uliojulikana Ukawa, walijiondoa baada ya Chadema kumpitisha Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.

Akizungumza na Mwananchi jana, Profesa Lipumba alisema, “Imekuwa kama surprise, sikutegemea kama Dk Slaa atateuliwa kwa sababu muda mwingi yupo Canada.”

Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema hana shaka na uteuzi huo kwa kuwa Dk Slaa ni mzoefu wa siasa na mzalendo ambaye ataitumikia vyema nafasi hiyo mpya.

“Narudia, sikutegemea. Ila popote atakapopangiwa kazi Dk Slaa atafanya kwa sababu najua ni mchapakazi,” alisema.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Rais Magufuli ana mamlaka kisheria ya kumteua mtu atakayemuona anafaa katika nafasi fulani.

“Huu ni uamuzi wa Rais sisi wengine hatuna comments zaidi ya kuwatakia kila heri katika utendaji wao wa kazi,” alisema Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza uteuzi huo wa Dk Slaa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema Rais Magufuli amemuonea huruma Dk Slaa ndiyo maana akaamua kumpa nafasi ya ubalozi.

Profesa Safari alisema hawezi kumsema vibaya Dk Slaa lakini nafasi hiyo ni huruma na zawadi ya Rais Magufuli.

Amedai Dk Slaa alijaribu kuivuruga Chadema wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 lakini hakufanikiwa.

“ Hii ni huruma. Siku zilizopita Dk Slaa aliandikwa katika vyombo vya habari kuwa anafanya kazi Super Market. Mimi nimekaa Ulaya najua maisha ya kule na Dk Slaa ni rafiki yangu sana lakini kwa kitendo alichokifanya mwaka juzi, haya ndiyo matokeo yake,” alisema Profesa Safari.

Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi kuanzia mwaka 2002 hadi 2008, Patrick Chokala alimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Dk Slaa kuwa balozi.

“Sina shaka hata kidogo na Dk Slaa ana uwezo wa kufanya kazi nchi yoyote. Hii kazi anaiweza na ni mtu mwenye dhamira ya kweli,” alisema Balozi Chokala.

Alisema anamfahamu Dk Slaa kwa kipindi kirefu tangu akiwa padre na kwamba, amekuwa ni mchapakazi hodari na mwenye hekima kwa watu.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam TV, Dk Slaa alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua ili aungane naye kujenga nchi na hivyo atafanya kazi kwa uwezo wake wote.

Dk Slaa ambaye hivi sasa anaishi Canada alisema, “Ni mapenzi ya Mungu, nashukuru kwa uteuzi. Ninachoweza kusema katika hatua hii, huu ni wajibu mkubwa kwenye kipindi cha kulijenga Taifa letu.”

Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search