Monday, 13 November 2017

MARAIS MAGUFULI NA MUSEVENI WALAANI MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA MAKOSA YA JINAI (ICC) KUANZA KUICHUNGUZA BURUNDI

Rais John Magufuli na Rais wa Uganda Yoweri Museveni wamelaani uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) wa kumuagiza Mwendesha Mashitaka wa Mahakama hiyo kuanzisha uchunguzi dhidi ya Burundi.

Marais hao walitoa kauli za kulaani uamuzi huo wakati wakiagana katika mji wa Masaka baada ya Rais Magufuli kukamilisha ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Uganda na kurejea nyumbani.

Baada ya kuagana Rais Magufuli alisindikizwa na Makamu wa Rais wa Uganda Edward Kiwanuka Sekandi hadi Mutukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda. Akizungumzia uamuzi huo wa ICC, Rais Magufuli alisema hatua hiyo inarudisha nyuma hatua zilizochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo iliunda Kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi inayoongozwa na Rais Museveni na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Benjamin Mkapa.

Alisema hali ya Burundi si mbaya kama inavyotangazwa kwa kuwa tayari wakimbizi wengi waliokuwa Tanzania wamerejea Burundi na wengine wanaendelea kurejea, na pia viongozi wanaosuluhisha mgogoro huo wamepanga kukutana Novemba 23, mwaka huu kwa lengo la kuendeleza mchakato wa kutatua mgogoro huo.

Kabla, Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) alisema ICC inaingilia mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kuwahusisha viongozi wa Jumuiya hiyo jambo ambalo si sahihi na linarudisha nyuma juhudi za kutafuta amani ya Burundi.

Majaji wa ICC walitoa uamuzi huo Novemba, 9, mwaka huu na kumtaka Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo kuchunguza vitendo vya kihalifu dhidi binadamu vilivyotokea nchini Burundi tangu ulipozuka mgogoro nchini humo miaka miwili iliyopita.

Shinikizo kutoka Mahakama ya ICC Juzi Mahakama ya ICC ilisema muda mfupi baada ya Burundi kuamua kujitoa katika taasisi hiyo, itachunguza madai ya kukiukwa kwa haki za binadamu katika nchi hiyo.

Taasisi moja ya Mahakama ya ICC ndiyo iliyotoa amri ya kufanyika kwa uchunguzi huo katika mji wa The Hague nchini Uholanzi ikidai kuwepo kwa madai ya mauaji, mateso, ubakaji na matukio mengine ya uhalifu.

Kwa mujibu wa Mahakama hiyo madai yatakayochunguzwa ni ya uhalifu uliotokea kati ya mwaka 2015 na 2017 ambapo Burundi ilikuwa mwanachama wa ICC. Uamuzi huo, kwa mujibu wa ICC ulipitishwa kabla ya Burundi kuamua kujitenga na Mahakama hiyo ya kimataifa.

Taarifa hiyo imesema uamuzi huo uliwekwa siri kwa sababu ya kuhakikisha usalama wa waathirika na mashahidi, hatua ambayo hata hivyo imetia shaka juu ya ukweli wa madai hayo ya Mahakama ya ICC.

Hata hivyo kabla ya Rais Magufuli na Rais Museven kulaani na kutoa msimamo huo wa pamoja tayari juzi serikali ya Burundi ilisema haitaruhusu uchunguzi huo ufanywe kama ICC inavyoshinikiza. 

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search