Friday, 17 November 2017

NDEGE YAANGUKA NA KUUWA WATU 11 HUKO ARUSHA

ABIRIA 10 na rubani mmoja wamepoteza maisha kwenye ajali ya ndege ya Kampuni ya Coastal Aviation.

Watu hao walikuwa wakisafiri ndani ya ndege aina ya Cessna Grand Caravan wakitoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda kwenye uwanja wa ndege wa Sorenera uliopo kwenye Hifadhi ya Serengeti mkoani Mara.

Ndege hiyo ilipata ajali leo majira ya saa tano asubuhi katika eneo la Bonde la Empakaai lililopo kwenye Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha. 

Kwa mujibu wa taarifa za ndani zilizothibitishwa, baadhi yao walikuwa ni watalii waliofika nchini kuona vivutio mbalimbali.

Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Charles Mkumbo alidhibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa hifadhi pamoja na usafiri wa anga.

“Ni kweli kuna ajali imetokea ya ndege, mahali ilipotokea ni eneo la bonde ambapo ni kama shimo fulani,” alisema Kamanda Mkumbo na kueleza kuwa maeneo hayo si rahisi kuyafikia wakati unapopata dharura.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Julian Edmunds alisema kuwa wameshtushwa na ajali hiyo na kusema kuwa: “Tumekuwa tukirusha ndege yetu mara kwa mara, tunaimani na marubani wetu lakini pia tunaimani na ndege yetu.

Kwa niaba ya kampuni ya Coastal tutakuwa tayari kushiriki kwenye uchunguzi wowote utakaohitajika kufanyika na hata ule unaoendelea. “Hakuna kitu muhimu kwetu kama usalama wa abiria wetu.

Maombi yetu kwa wote walioguswa na tukio hilo na kwasasa tunaendelea kuchunguza na tutatoa taarifa zaidi zitakapojitokeza,” alisema Mkurugenzi huyo. Hata hivyo taarifa za awali zinasema kuwa ndege hiyo iligonga mlima na kuanguka kwenye bonde hilo baada ya kupata hitilafu.

Ajali hii inakuja ikiwa ni wiki tatu tangu ilipotokea ajali nyingine ya ndege nyingine ya Coastal ambapo watalii wawili walijeruhiwa huku wengine tisa waliokuwa kwenye ndege hiyo wakitoka salama.

Tukio hilo la ajali lilitokea Oktoba 25, 2017 saa tisa alasiri wakati ndege hiyo ilipokuwa ikitua Serengeti, na chanzo cha ajali hiyo ilitajwa kuwa ni mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha na kusababisha uwanja kujaa maji

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search