Saturday, 11 November 2017

SETH APEWA MASHARTI HAYA KWENDA KUTIBIWA NJE

Masharti Aliyopewa Sethi ili Aweze Kutibiwa Nje
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,jijini Dar es Salaam, imemtaka mfanyabiashara Harbinder Seth, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kutakatisha fedha, awasilishe  maombi ya kwenda kutibiwa nje ya nchi Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Kadhalika, imeruhusu upande wa Jamhuri kwenda kuwahoji washtakiwa mahabusu kwa ajili ya kuendelea na hatua za kukamilisha upelelezi.

Uamuzi huo ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili za kesi hiyo.
Kabla ya uamuzi huo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Leonard Swai, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Joseph Sungwa, alidai kuwa mshtakiwa Sethi ameona Hospitali ya Muhimbili haina uwezo wa kumtibu maradhi yake na kwamba anaomba daktari wake kutoka Afrika ya Kusini aitwe aje nchini au apelekwe nchini humo chini ya ulinzi kwa ajili ya afya yake.

Akijibu hoja za utetezi, Swai alidai kuwa Muhimbili haijasema kwamba haiwezi kumtibu mshtakiwa bali anajichelewesha kwa kumtaka daktari kutoka Afrika Kusini.

Pia aliomba utaratibu wa Jeshi la Magereza uheshimiwe kuhusu mshtakiwa kupata huduma za matibabu na kwamba Sethi kupelekwa Afrika Kusini akiwa chini ya ulinzi haiwezekani.

"Mheshimiwa upande wa Jamhuri tunaomba kibali cha kwenda kuwachukua washtakiwa maelezo ya onyo ili kukamilisha upelelezi," alidai Swai.

Hakimu Shaidi alisema mahakama yake ilitoa amri ya mshtakiwa kwenda kupatiwa matibabu Muhimbili na amepata na kuhusu daktari wake kutoka Afrika Kusini, awasilishe maombi Mahakama Kuu na upande wa Jamhuri umekubaliwa kwenda mahabusu kuchukua maelezo ya washtakiwa.

Sethi na mshtakiwa mwingine James Rugemarila kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi, kutakatisha fedha  na kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Kesi imepangwa kutajwa Novemba 24,mwaka huu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search