Thursday, 16 November 2017

VITENDO VYA KISHIRIKINA WALIMU SABA WAJIKUTA WAMELALA NJE HUKU SEHEMU ZAO ZA SIRI ZIKIWA ZIMENYOLEWA


Walimu saba wanaofundisha Shule ya Msingi Soswa wilayani Sengerema mkoani Mwanza wamejikuta wamelala nje pamoja na familia zao huku wawili kati yao wakiwa wamenyolewa nywele kichwani na sehemu za siri.


Mwalimu wa Shule ya Msingi Soswa, Petro Lukas amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamukia leo Jumatano ambapo walimu hao walipokuwa wamelala ndani ya nyumba zao na walipotahamaki usiku walijikuta wamelala nje.


Amesema palipokucha walimu hao walizinduka na kutokuamini kilichotokea na walipoingia ndani ya nyumba zao walikuta damu zimetapakaa vyumbani na sebuleni pia vibuyu vikiwa vimevalishwa shanga nyeupe vikiwa kitandani na chini kitendo kiliwafanya kuhaha kuomba msaada kwa jamii inayowazuguka.


Mwalmu Lukas amesema kati ya walimu hao wawili wameathirika zaidi na tukio hilo na kwa kupata mshituko ambao ni Wape Kisumo aliyenyolewa nywele kichwani pmaoja na Daud Shule ambaye alinyolewa nywele sehemu za siri.


Kutokana na mshtuko huo Kisumo alipelekwa kituo cha afya cha Mwangika kwa matibabu na mwalimu Shule yeye anaendelea na matibabu ya tiba na hali zao zinaendelea vizuri.


Mganga Mkuu Halmashauri ya Buchosa, Dk Ernest Chacha amekiri kumpokea mwalimu Kisumo katika kituo cha afya Mwangika na kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu na baada ya uchunguzi wa kitaalamu kukamilika watatoa taarifa lakini alipofika kituoni alikuwa haongei ila baada ya kupatiwa huduma ya kwanza ameanza kuongea kidogo.


Akizungumzia mkasa huo mwalimu Shule amesema kuwa wao baada ya kupata chakula cha usiku walilala ndani nyumba zao na ilipofika usiku wa manane wakasikia mwalimu mwenzao Wape Kisumo akilia na kulalamika kichwa kinamuuma.


Amesema walipotahamaki walijikuta wakiwa nje watupu na kuona kuwa wamedhalilishwa na kitendo hicho hivyo wanaiomba Serikali iwasaidie kumaliza tatizo hilo.


Mmoja wa wananchi wa Kisiwa cha Soswa, Sumari Diplospa amesema kitendo hicho kinapaswa kukemewa kwa kuwa walimu hao wanasaidia kufundisha watoto wao.


Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bulyaheke Musa Mwilomba amesema kuwa tukio hilo ni tatu kutokea katika shule hiyo ambapo mwaka jana mwezi nne walimu walipondwa mawe nyumba zao wakiwa wamelala.


Pia Mei 5 mwaka huu nyumba za walimu zilipondwa tena mawe na usiku wa kuamkia leo wamejikuta wamelala nje na baadhi yao kunyolewa nywele sehemu za siri kitendo ambacho kinapaswa kukemewa.


Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Buchosa, Magareth Kapolesya amesema amepata taarifa ya tukio hilo na kusikitishwa na kitendo hicho na wao kama wasimamizi wa elimu watalishughulikia na kupata ufumbuzi juu ya suala hilo kwa kuwa linawanyima raha walimu na kukosa morali ya kufundisha.


Imeandaliwa na Daniel Makaka - Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search