Wednesday, 8 November 2017

VYAMA VINNE VYAUNGANA NCHINI LIBERIA KUPAMBANA NA GEORGE WEAH

Vyama vya Siasa Vinne Vyaungana Kumpinga Weah Kuwa Rais


Vyama vinne vya siasa Jumanne vilifanya mazungumzo ili “kuungana” kwa lengo la kumpa uwezo makamu wa rais Joseph Boakai kupambana dhidi ya mchezaji soka nyota wa zamani wa kimataifa George Weah kuwania kiti cha urais wa Liberia.

Ofisa wa ngazi ya juu wa chama tawala cha Unity Party (UP) alisema mazungumzo hayo yalifanyika siku ambayo wananchi wa Liberia walipaswa kupiga kura katika uchaguzi wa marudio kati ya Weah aliyeongoza duru ya kwanza kwa asilimia 38 na Boakai aliyeshika nafasi ya pili akiwa na asilimia 28.

Uchaguzi huo wa marudio haukufanyika kama ilivyopangwa baada ya Mahakama ya Juu, Jumatatu kuiweka Liberia kwenye njiapanda ilipositisha kwa muda usiojulikana, na wadadisi wa masuala ya siasa wanasema unaweza kucheleweshwa kwa wiki kadhaa.

Mahakama iliamua uchaguzi usiendelee hadi yatakapotatuliwa malalamiko kuhusu ulaghai katika mchakato yaliyowasilishwa na chama cha Liberty Party ambacho mgombea wake ni Charles Brumskine.

Mwenyekiti wa UP, Robert Kpadeh alisema mazungumzo yalihusu vyama vinne vilivyoweka wagombea urais akiwemo Brumskine, ambaye alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa Oktoba 10 na walijadili “kuunganisha nguvu katika Nyanja mbalimbali."

"Unachokiona leo ni ishara kubwa kwa ulimwengu kwamba wanakuja pamoja kwa lengo la kupigania demokrasia,” alisema Kpadeh.

"Tunaamini kabisa kwamba Weah hawezi kuongoza nchi."

Alipoulizwa ikiwa vyama hivyo vitamfanyia kampeni Boakai iwe kwa uchaguzi wa marudio ikiwa hatimaye utafanyika, Kpadeh alijibu: "Inawezekana" akasisitiza kwamba vyama hivyo vinne vimekubaliana kusimamia pamoja kesi dhidi ya ulaghai.

Oktoba 23 Brumskine alifungua kesi akilalamikia "ulaghai mkubwa na dosari" uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akidai kuzikwa kwa baadhi ya makaratasi ya kupigia kura na kujaa kadi za kidanganyifu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search