Thursday, 2 November 2017

Wizara: Ni sahihi kuchoma vifaranga na utaratibu unatambulika kimataifa, yarusha lawama kwa waliosambaza picha

Wizara ya mifugo na uvuvi imetetea uamuzi wa kuchoma vifaranga kwani ni utaratibu unaotambulika kimataifa na kwa mujibu wa sheria namba 17 ya sheria ya wanyama ya mwaka 2003 imechukua uamuzi huo wa kuteketeza vifaranga hivyo 6400 ili kuepusha kusambaza mafua ya ndege.

Msimamo huo umetolewa na katibu mkuu wa wizara, amesema hatua hio imefikiwa kuzuia kuenea ugonjwa wa aina yoyote wa kuku kuingia kwenye kuku wa nchini na kuzuia uingizaji holela wa vifaranga bila kupitia utaratibu na sheria zilizopo.

Amesema hasara ambayo ingeletwa na vifaranga 6400 kama wangeingia kwa namna waliyoingia na kuleta madhara yangekuwa makubwa zaidi kuliko yanayoonekana kwa kuteketeza vifaranga 6400.

Alipoulizwa kama hakukuwa na namna nyingine ya kuviaribu zaidi ya kuviteketeza hadharani, amesema havikuchomwa hadharani na amesema waliosambaza hizo picha walikuwa na lengo tofauti, amesema vitu vinavyofanyika nje ya hadhara maana yake havitakiwi kuonekana kwenye hadhara na mtu akikiuka ndio analeta madhara kama yaliyotokea.

Amesema utaratibu wa kuwachoma umetumika pia na mataifa mengine akitolea mfano Ulaya kilipotokea kichaa cha Ng'ombe lakini amesema sio kitendo cha kumuonyesha kila mtu ndivyo walivyofanyiwa.

Kuhusu kuwapima, amesema hawawezi kupima vifaranga ambavyo tangu awali walishatoa katazo visiingie nchini.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search