Thursday, 7 December 2017

ALIYEKUWA MWENYEKITI WA CCM MKOA WADAR ES SALAAM APANDISHWA KIZIMBANI KWA KESI YA UHUJUMU UCHUMI

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano jana Jumatano walipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi ikiwamo kusambaza dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi ' ARV’s ' na kusababisha hasara ya Sh 148 milioni.


Kabla ya kusomewa mashtaka ya kesi hiyo mpya ya uhujumu uchumi namba 80 ya 2017, mahakama ilimfutia kesi iliyokuwa na mashtaka matano yanayofanana na hiyo iliyofunguliwa mwaka 2014.


Kesi hiyo ilifutwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa baada ya Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro kuomba iondolewe kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.


Kesi hiyo ilikuwa katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na mashadi tisa walikuwa wamekwishatoa ushahidi wao na washtakiwa walikuwa nje kwa dhamana.


Baada ya kesi hiyo kufutwa, Madabida ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa kiwanda hicho na wenzake walikamatwa tena na kufunguliwa kesi hiyo mpya ya uhujumu uchumi.


Mbali na Madabida wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Seif Shamte ambaye ni mkurugenzi wa uendeshaji, Simon Msoffe (meneja masoko) na Fatma Shango (mhasibu msaidizi) wa Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd. Pamoja na Sadick Materu na Evans Mwemezi ambao ni maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa. 


Baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa hao hawakurusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.


Wakili wa Serikali, Pius Hilla alisema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika lakini DPP bado hajafanya maamuzi kama isikilizwe Kisutu ama Mahakama Kuu.


Washtakiwa hao wanatetewa na Mawakili Denis Msafiri, Makaki Masatu na Nehemiah Nkoko.


Wakili Msafiri alisema Mahakama ya Kisutu inayo mamlaka ya kuisikiliza hiyo kwa sababu kiwango chake cha fedha kipo chini ya Sh 1 bilioni ambayo ndiyo inapaswa kusikilizwa Mahakama Kuu.


Kutokana na hoja hiyo Wakili Hilla aliomba wapewe muda hadi leo Alhamisi ndiyo wajibu hoja ya upande wa utetezi.Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi leo Alhamisi kutokana na ombi hilo na kuamuru washtakiwa wapelekwe polisi hadi leo Alhamisi itakaposikilizwa hoja kama mahakama hiyo ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ama la.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search