Wednesday, 13 December 2017

CCM YAFUTA MCHAKATO WA KURA ZA MAONI JIMBO LA NYALANDU

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefuta mchakato wa kura ya maoni jimbo la Singida Kaskazini.Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 12,2017 amesema mchakato huo utarudiwa.


Amesema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa mamlaka aliyonayo kikatiba na kikanuni ameufuta mchakato huo kutokana na baadhi ya wagombea bila haya, soni, aibu na kinyume na misingi yote ya CCM wamejihusisha na vitendo vya rushwa.


Kutokana na hilo, amesema kesho Jumatano Desemba 13,2017 saa mbili asubuhi hadi saa 12:00 jioni wanachama wa CCM wanaotaka kugombea jimbo la Singida Kaskazini wachukue fomu na kuzirejesha.


Polepole amesema Alhamisi, Desemba 14,2017 itapigwa kura ya maoni na halmashauri kuu ya jimbo badala ya mkutano mkuu wa jimbo ili kuwahi mchakato.


Taarifa hiyo imesema Haider Gulamali na Elia Mlangi hawaruhusiwi kugombea nafasi hiyo kupitia CCM kutokana na tuhuma nzito za kujihusisha na vitendo vya rushwa.


“Wana CCM hawa wawili suala lao liko mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa –Takukuru,” imesema taarifa hiyo.


Polepole amesema wana CCM wengine waliojihusisha kwa namna moja au nyingine kutoa au kupokea rushwa wanaendelea kuchunguzwa na vyombo vya chama hicho vyenye dhamana ya udhibiti wa nidhamu, usalama na maadili pamoja na vingine vya dola vya kiuchunguzi.


CCM imesema wanachama wengine waligombea isipokuwa hao wawili wanaruhusiwa kufuata utaratibu wa kuomba ridhaa kwa namna ilivyoelekezwa.


Imeelezwa Kinana atateua kiongozi au ofisa mwandamizi atakayekwenda kusimamia mchakato wa kura ya maoni katika mkutano wa halmashauri kuu ya jimbo la Singida Kaskazini.


Chanzo - Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search