Wednesday, 6 December 2017

IGP Sirro: Tumetuma makachero Nairobi kumhoji Lissu na dereva wake

Image result for sirro
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, amesema timu ya wapelelezi imetumwa kwenda Nairobi, Kenya kufanya mahojiano na Tundu Lissu.

MKUU WA JESHI LA POLISI NCHINI IGP, SIMON SIRRO

Mbali na Mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema), timu hiyo pia itafanya mahojiano na dereva na mlinzi wake, imeelezwa. 

Tangu Lissu ashambuliwe kwa risasi 32 na watu wasiojulikana mchana wa Septemba 7, mwaka huu nje ya nyumba yake Area D mjini Dodoma wakati akitoka bungeni, Polisi ilikuwa haijafanya naye mahojiano.

Aidha, dereva wake, Simon Bakari amekuwa akitajwa na polisi kama mtu muhimu anayeweza kusaidia upelelezi.Hata hivyo Bakari amekuwa Kenya tangu siku hiyo pamoja na Lissu ambaye amelazwa kwenye Hospitali ya Nairobi baada ya risasi tano kumpata maeneo mbalimbali ya mwili wake. 

Akizungumza jana na Nipashe katika mahojiano maalum, IGP Sirro alisema wametuma wapelelezi Nairobi baada ya kusikia Lissu amekubali kuhojiwa juu ya tukio hilo na matarajio yao pia ni kuwapata dereva na mlinzi wake.

“Tumetuma watu wetu kwenda kuchukua maelezo yake (Lissu)," alisema IGP Sirro. "Mwanzo tuliomba kwenda lakini chama (Chadema) walikataa. Juzi tumesikia wamesema wapo tayari".

"Tumetuma vijana wetu wawili kwenda Nairobi kuchukua maelezo yake.”

Alisema lengo kubwa ni kujua mazingira ya shambulio yalikuwaje na kwamba ikiwezekana wampate dereva na msaidizi huyo wa Lissu ili kurahisisha upepelezi wa tukio lenyewe.

“Upelelezi unaingia vitu vingi sana (sasa) kutompata dereva na mlinzi wake Lissu inashindwa kutupa picha kamili ya tukio,” alibainisha.

“Niwaambie Watanzania watuamini, hatuko kwa ajili ya kuona hatumtendei mtu haki, tupo kwa ajili ya kutenda haki.”Mara baada ya Lissu kupigwa risasi, Bakari alikuwa mmoja wa watu waliompeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kisha kupanda naye ndege iliyompeleka Nairobi usiku huo kwa matibabu zaidi.

Kutokana na kusafiri na Lissu, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma liliagiza ajisalimishe haraka iwezekanavyo kwa ajili ya uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari siku mbili tangu kushambuliwa kwa Lissu, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alimtaka Bakari ajisalimishe polisi.

"Polisi inamtaka dereva wa Tundu Lissu ajitokeze na afike Polisi Dodoma bila kukosa au Makao Makuu ya Upelelezi (ofisi ya DCI) Dar es salaam ili aweze kutoa maelezo,” alisema Muroto Septemba 9.

“Kutoweka kwake na kujificha ni kosa la jinai na kama kuna mtu au watu wanamficha wanatenda kosa la jinai."Wamfikishe Polisi bila kukosa kwa kuwa ni shahidi muhimu katika upelelezi.”

WANATAKA TUKAMATE

Kwa mujibu wa IGP Sirro, mhalifu anaweza kuwa hata mke ndani ya nyumba kwa kuwa kuna matukio ya mama kukodisha watu wa kumuua mume.

“Tukimpata (dereva wa Lissu) tutashukuru," alisema IGP Sirro "kwani inakuwa sasa hata dereva anajificha"."Wanataka tukamate watuhumiwa wakati wao (dereva na mlinzi) wanaoweza kuwa mashahidi, nao hatuwapati.

“Sasa itakuja kuwa msaidizi wake (Lissu) wa kawaida, suala ni upelelezi ndiyo utatuambia ukweli, lakini kutompata msaidizi wake; anafichwa.

"Yeye mwenyewe (Lissu) kwa sababu sasa ameruhusu ngoja vijana wetu waende wahoji na nitashukuru kama chama (Chadema) kitatusaidia kumpata dereva na mlinzi tumuhoji tujue majibu ni nini.”

Kuhusu kuundwa kwa timu huru ya kuchunguza shambulio itakayohusisha vyombo vya usalama vya nje, IGP Sirro alisema Watanzania watambue kuwa jeshi lake lina uwezo wa kufanya kazi hiyo na halijashindwa.

“Kama matukio ya (mauaji ya) Kibiti yamefika hapa yalipo, tumewapata wahalifu, itakuja kuwa habari ya Lissu? Walikufa wengi kule Kibiti mbona hatukusema Watanzania watafute timu huru?”

Hata hivyo, IGP Sirro alisema kama utaratibu unaruhusu kuwepo kwa timu huru ya uchunguzi, upande wa Lissu uangalie utaratibu wa kufanya hivyo kwa kuwa polisi haina pingamizi.

“Tunachojua tumepewa dhamana ya kupeleleza kesi mbalimbali, kama wana uwezo na sheria inawaruhusu sina pingamizi na hilo,” alisisitiza IGP Sirro.

Tangu kutokea kwa tukio hilo hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na jeshi hilo ambalo awali lilikamata magari nane aina ya Nissan Patrol, meupe, yaliyokuwa kwenye viunga vya Dodoma Septemba 7.

Juzi familia ya Lissu iliieleza Nipashe kuwa wakati wowote Mbunge huyo atasafirishwa kwenda nchi za Ulaya Magharibi kwa ajili ya mazoezi ya viungo yatakayomwezesha kurejea katika hali yake ya kawaida.

CHANZO: Nipashe

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search