Monday, 4 December 2017

KUGHUSHI NAMBA ZA SIMU KWAWAPANDISHA KIZIMBANI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewafi kisha mahakamani watu watatu, wakituhumiwa kughushi kwa kubadilisha namba tambulishi za simu za mkononi.

Mwanasheria Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Johannes Kalungula aliwataja washitakiwa hao jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Wilbert Chuma kuwa ni mkazi wa Mkuyuni wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, Daudi Masesa na mkazi wa Nyashana wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Isaya Daudi Lucas (31).

Mwanasheria mwingine wa TCRA, Emma Gelani alimtaja mshitakiwa mwingine mbele ya Hakimu Mkazi, Sumaye wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana kuwa ni mkazi wa Nyamanoro wilayani Ilemela, Faraji Said Faraji.


Kalungula aliiambia Mahakama kuwa Agosti 17, mwaka huu, Masesa akiwa eneo la Rwagasore wilayani Nyamagana alijaribu kubadili namba tambulishi 35772087347213 na 354773087347211 za simu aina ya Samsung Galaxy J7 Prime yenye namba za usajili R58J61EY6SJ. Pia alibadili namba tambulishi 358476052431913 ya Samsung Galaxy Note 3 yenye namba za usajili RF8F- 10FLWA kuwa na namba tambulishi 351776065482262.


Aliongeza kuwa siku na tarehe hiyo hiyo, Lucas akiwa eneo la Ngolo wilayani Nyamagana, alibadili namba tambulishi 357201081915202 na 357201081915210 za Tecno Cx Air yenye namba za usajili SN 023811075040117 kuwa 357901081915207 na 357901081915215.


Kwa upande wake, Mwanasheria Gelani aliiambia Mahakama kuwa siku hiyo hiyo, mshitakiwa Faraji akiwa eneo la Lumumba wilayani Nyamagana, alifanya jaribio la kubadili namba tambulishi 354772087325086 na 354773087325084 za Samsung Galaxy J 7 PRO yenye namba za usajili R58J61EW5QT.

Washitakiwa hao walitenda makosa hayo kinyume cha Kifungu cha 135 cha Sheria ya Namba 3 ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya Mwaka 2010. Hata hivyo, washitakiwa walikana kutenda makosa hayo na kesi hiyo kuahirishwa hadi Desemba 18, mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo. 

Washitakiwa hao waliachiwa kwa dhamana, ambapo Masesa alidhaminiwa na watu wawili kwa Sh milioni 10, Lucas mdhamini mmoja kwa Sh milioni nane na Faraji wadhamini wawili.
Chanzo- Habarileo

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search