Wednesday, 13 December 2017

Mabilioni ya Hela Yakamatwa Yakiingizwa Nchini Kinyume cha Sheria

Mabilioni ya Hela Yakamatwa Yakiingizwa Nchini Kinyume cha Sheria
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema zaidi ya dola bilioni moja zimeshikwa zikiingizwa nchini kwenye uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam.

Akiwa jukwaani mjini Dodoma leo wakati akizindua tawi la Benki ya CRDB, Rais Magufuli ameweka wazi kuwa amepata taarifa zaidi ya kiasi cha dola bilioni moja zimeshikwa zikiingizwa nchini kinyume na sheria kupitia uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam.
“Ninapozungumza tu sasa hivi nimepata taarifa zaidi ya bilioni moja dola zimeshikwa Airport zilikuwa zinaingizwa Tanzania kwasababu Tanzania kimeshaonekana ni kichaka cha fedha za kigeni” amesema Rais Magufuli.

Kwa upande mwingine Rais amezitaka mahakama za biashara nchini kuharakisha kesi zinazohusiana na kesi za mikopo ili kuwezesha Benki kuendelea kutoa mikopo. Pia ameongeza kuwa baadhi ya wakopaji hutumia fedha hizo hizo za mikopo kuchelewesha kesi, hivyo mahakama zinatakiwa kutoa hukumu kwa wakati.
“Nawahimiza wananchi kulipa madeni yao kwa wakati, dawa ya deni kulipa, na niziombe Mahakama za biashara kuharakisha kesi zinazohusu mikopo, mtu anapopelekwa amekopa na anatakiwa kuuziwa jengo lake au kufirisiwa, unachelewesha nini toa amri watu wakauze ilikusudi Benki ziendelee kukopesha wengine”, amesema Magufuli.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search