Monday, 11 December 2017

MAGUFULI AWAPONDA UVCCM

Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli akisalimiana na baadhi ya wanachama wapya wa chama hicho.

****


RAIS John Magufuli amepigilia msumari kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis akidaiwa kutoa rushwa akisema atashangaa kama atachaguliwa mwenyekiti anayewahonga fedha wamchague.

Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge alikamatwa jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dodoma. 

Alikamatwa kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa umoja huo akiwa nyumbani kwake maeneo ya mnada wa zamani wa Manispaa ya Dodoma.

Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Emma Kihanga alithibitisha kukamatwa kwa Sadifa na kusema watatoa taarifa baadae kuhusu hilo. 

Kwenye mkutano wa tisa wa UVCCM, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa alisema kijana mpenda rushwa, mwizi, fisadi na tapeli ana mchango mdogo kwa Taifa na hana tija.

“Ninavyozungumza hapa Mwenyekiti wenu yuko mahabusu kwa tuhuma za rushwa, huo ndiyo umoja wa vijana?... lakini lazima niwaeleze, umoja wa vijana tuliokuwa tunaujua na mimi nilikuwa mwanachama, siyo muelekeo uliopo sasa.

“Umoja huu baada ya nchi kupata uhuru ilikuwa ni chachu ya kuwavuta wananchi kujiunga na chama, ilikuwa sauti, mtete na chemchem ya fikra mpya na chuo cha vijana kuandaliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi,” alisema.

Rais Magufuli alisema pamoja na kwamba anajua vijana walifanya kazi kubwa mpaka akaingia madarakani, lakini hakupelekewa orodha ya majina kutoka UVCCM wakati akiteua viongozi katika ngazi mbalimbali.

Alisema anatambua vijana wa CCM ndiyo viongozi wa kesho, hivyo alitumia mbinu zake mbadala kuwapata vijana aliowapa nafasi aliopata wasifu wao kupitia njia mbalimbali. “Wengi walikosa nafasi kupitia umoja wa vijana, nazungumza haya ili mpate nafasi ya kufanya mabadiliko Umoja wa Vijana, msirudie makosa na mtambue jukumu lenu kwenye taifa hili na kwa vijana wa vyama vyote,” alisema.

Alisema viongozi wa vijana wanaochaguliwa hapo ndiyo watakuwa washauri wake. Alisema jumuia hiyo ina mali nyingi lakini zinatumika ovyo na wamekuwa viongozi ambao wakati wa uchaguzi wanawekwa mifukoni na wagombea.

“Mnakipeleka chama pabaya, mnatengeneza makundi ambayo hayatusaidii kama nchi. Nawaomba mchague viongozi wanaofaa msije kuliangusha taifa,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema UVCCM imekuwa kundi la kuwazuia watu wasiingie CCM kwa kuwawekea vigingi watu wenye uwezo na mapenzi mema na chama. Rais Magufuli alisema vijana walioamua kurudi CCM huko nyuma waliwahi kunyimwa nafasi ya kujiunga na umoja huo hivyo wakaamua kuondoka lakini sasa wameamua kurudi.

“Inawezekana wengine walijitahidi lakini wakakuta vizingiti, ninawaomba msitengeneze vizingiti, umoja wa vijana uwe kimbilio la vijana,” alisema. Alisema bado ana imani kubwa na vijana na wengi ambao amewachagua kushika nafasi mbalimbali za uongozi hawajamuangusha.

Alisema ndani ya chama hicho sasa anahitaji vijana wanaochukia ufisadi, wanaoweza kutetea nchi, ambao hawataweza kununuliwa na mtu. Aliwataka vijana kuchagua viongozi ambao siyo wala rushwa na siyo kwa kufuata ukabila bali wachague viongozi madhubuti wanaotanguliza maslahi ya taifa mbele kwani chama hicho ni chama kinachojitambua chenye maadili mema.

Aliwataka vijana kujitambua kwani wakati wa kushika dola ni sasa lakini asingependa kuacha nchi kwa viongozi wala rushwa kwani itakuwa ni usaliti kwa nchi na waasisi wa nchi hii, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume.

“Mimi ni Rais lakini siyo Rais wa maisha yote, nafasi hizi za uongozi ni zetu vijana lakini tusingependa tunapoondoka tunamuachia kijana mla rushwa,” Rais Magufuli aliwaambia vijana. Alisema anawatambua vijana wenye uwezo ndani ya chama hicho na atahakikisha anatoa nafasi za uongozi kwa vijana ambao wana uwezo na utaalamu mbalimbali ndani ya chama hicho.

Aliwataka pia vijana kuendelea kujibu hoja mbalimbali zinazoandikwa na watu kwenye mitandao ya kijamii kwa upotoshaji. Kuhusu mali za UVCCM, Rais Magufuli alisema mali za umoja huo zimekuwa zikitumika ovyo ikiwemo viwanja na majengo na akawataka watakaochaguliwa wasibweteke bali waanzishe miradi na kwamba haoni kama kuna ugumu wa kuwa na miradi mikubwa.

“Kigugumizi kilikuwepo utampa nani huu mradi utapona? kama jengo la umoja wa vijana la Dar es Salaam haijulikani kiasi gani kinaingia kila mwaka, kuna wengine wamekabidhiwa vyumba vyao, kuna petrol station Songea hawajui fedha zinaingia kwa nani,” alisema Rais Magufuli.

“Mmekuwa na viongozi ikifika wakati wa uchaguzi wamekuwa wakiwekwa mfukoni na wagombea, tunakipeleka chama pabaya tunatengeneza magumu ambayo hayatusaidii nchi hii, naomba vijana chagueni kwa kufikiria A-Z ili msije kuliangusha Taifa,” alisema kuhusu viongozi UVCCM kuwekwa mfukoni.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia alisisitiza kuwa kuhamia kwake CCM ilikuwa ni uamuzi wake binafsi na siyo kwamba amenunuliwa na Rais Magufuli kama watu wanavyoeneza.

Alikiasa chama kujiandaa kwa uchaguzi mdogo wa marudio katika majimbo mbalimbali hasa Kinondoni, Dar-es-Salaam ili jimbo hilo liende CCM na kuongeza idadi ya majimbo wanayomiliki kutoka manne na kuwa matano.

Aliyekuwa mbunge wa Kigoma kusini (NCCR), David Kafulila alisema sababu kubwa ya kujiunga CCM ni uwepo wa Utu na Usawa ndani ya chama hicho na ajenda ya ufisadi aliyokuwa anaipigania wakati akiwa upinzani kuhama na kubebwa na kutekelezwa na CCM.

Aliyewahi kuwa mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali alisema ameamua kujiunga na CCM ili kujiunga na timu ya ushindi. “Zimepigwa propaganda nyingi, Rais utasemwa maneno mengi kuwa unawanunua wapinzani, huo ni udhaifu na wanaosema hivyo ni wadhaifu na tusiruhusu watu wachache kutumia propaganda za kudhuru taifa letu,” alisema.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search