Monday, 4 December 2017

MBEGU ZA MAHINDI FEKI ZASAMBAA MIKOANI

Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba ameitaja mikoa ya Rukwa, Njombe, Iringa, Songwe na Mbeya kuongoza kwa kuuza mbegu feki za mahindi na kusababisha madhara makubwa kwa wakulima, ikiwemo uzalishaji mdogo wa zao hilo.

Kutokana na hatua hiyo, Waziri Tizeba ameiagiza Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu bora nchini (TOSCI), kukagua maduka yanayouza pembejeo za kilimo yakiwemo mahindi katika mikoa hiyo ili wajiridhishe kama yamesajiliwa na taasisi hiyo na uhalali wa mbegu za mahindi wanazowauzia wakulima kama ni bora.

Aidha, ameagiza wafanyabiashara wanaouza pembejeo za kilimo, wakibainika kuuza mbegu feki za mahindi, wafungiwe maduka yao, wanyang’anywe leseni zao za biashara na kufikishwa mahakamani, akisisitiza kuwa uhaba wa mbegu bora uliopo nchini, hauwezi kuwa kigezo cha wafanyabiashara wasio waaminifu kuuza mbegu feki za mahindi.

Tizeba alitoa maagizo hayo jana, alipomtembelea mkulima mkubwa, Salum Sumry katika shamba lake la Msipazi Farm lililopo Kijiji cha China wilayani Nkasi mkoani Rukwa, ambapo alielezwa kuwa mbegu feki ni janga kubwa mkoani humo.

“Hii haiwezi kuvumilika mikoa hiyo mitano ikiwemo Mkoa wa Rukwa ni vinara wa kuuza na kusambaza mbegu feki kwa wakulima mbaya zaidi kwa wakulima wadogo. “Wanachofanya wafanyabiashara wa mbegu za mahindi wanapaka mbegu hizo rangi za mikeka na kuziweka kwenye vifungashio bandia kisha wanawauzia wakulima. “Kwa kufanya hivyo wanasababisha wazalishaji wa zao hili kukata tamaa kwani madhara yake ni makubwa sana.

Badala ya kuvuna magunia 20 kwa hekta moja wanabakia kuambulia magunia manne tu,” alisema Waziri Tizeba.

 Alisema mahindi hayo yanatoka nchini Zambia kupitia mji mdogo wa Tunduma uliopo mpakani na kuuzwa mkoani Songwe, ambapo bei ya kifungashio cha kilo 12 ni hadi Sh 7,000 ambayo ni mara saba ya bei halali.

Aidha alisema bei ya rejera ya mahindi mkoani Rukwa, imeporomoka katika msimu huu wa kilimo kutoka Sh 100,000 kwa gunia lenye uzito wa kilo 100 hadi kufikia Sh 30,000, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosa soko la uhakika hatua inayowakatisha tamaa wakulima.

 Katika taarifa yake, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alimweleza Tizeba kuwa mahindi hulimwa kwa wastani wa asilimia 43 ya mazao yote yanayolimwa kila mwaka mkoani humo.
IMEANDIKWA NA PETI SIYAME - HABARILEO SUMBAWANGA

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search