Wednesday, 6 December 2017

MWANDISHI WA HABARI WA GAZETI LA MWANANCHI APOTEA KATIKA MAZINGIRA YA KUTATANISHA

Mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda amepotea.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na mkurugenzi mtendaji wa MCL, Francis Nanai ilisema Novemba 30, kampuni ilipokea taarifa za kutoonekana Azory kwa siku tisa.

Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinoni (35), Novemba 21, asubuhi watu wanaokadiriwa kuwa wanne wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walifika katikati ya mji wa Kibiti sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara na kumchukua.

Katika taarifa hiyo imeelezwa baada ya kumchukua Azory, gari hilo lilielekea shambani kwake saa nne asubuhi na kumkuta mkewe Anna akiwa huko.

Imeelezwa Azory aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma alimuita mkewe kutokea upande huo wa gari na kumuuliza alikokuwa ameuweka ufunguo wa nyumba yao.

Taarifa ilisema mkewe alilisogelea gari na kuzungumza naye kutokea dirishani na kumwelekeza alipoficha ufunguo, huku Azory akimwambia amepata safari ya dharura na kama asingerudi siku hiyo Novemba 21, basi angerudi siku inayofuata Novemba 22.

Nanai katika taarifa hiyo, alisema gari hilo liliondoka kwa kurudi kinyumenyume hadi njia panda na kuelekea nyumbani kwa mwandishi huyo.

“Mkewe aliporudi nyumbani aligundua kuna upekuzi ulifanyika kwa sababu alikuta vitu viko shaghalabaghala,” inasema taarifa hiyo.

Tangu siku hiyo, imeelezwa Azory hajaonekana na namba zake tatu za simu za mkononi hazipatikani. Mpaka jana amefikisha siku 14.

Novemba 23, mkewe Anna alitoa taarifa kituo cha polisi Kibiti na kupewa RB namba; Kibiti/RB/1496/2017.

Imeelezwa polisi waliahidi kufanya uchunguzi, lakini mpaka sasa hakuna taarifa zilizotolewa.

Taarifa ilisema kwa mara ya mwisho, Azory aliwasiliana na ofisi za Mwananchi Novemba 20 kwa majukumu ya kikazi.

Nanai alisema MCL inafuatilia suala hilo kwa ukaribu kwa kushirikiana na familia yake na kutoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa haraka ili kuwezesha kupatikana kwa mwandishi huyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Onesmo Lyanga alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema bado hajapata taarifa za kupotea kwa mwandishi huyo.

“Sina taarifa, ndio kwanza nasikia kutoka kwako kama Gwanda amepotea. Lingekuwa tukio la crime (uhalifu) wasaidizi wangeshaleta taarifa lakini hili la kupotea sijalipaata,” alisema Kamanda Lyanga.

Alisema kama mkewe ameshatoa taarifa polisi amefanya jambo zuri kwa kuwa zitashughulikiwa.
Chanzo- Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search