Monday, 18 December 2017

Takukuru Yatupilia Mbali Ushahidi wa Nassari, Lema

Takukurua Yatupilia Mbali Ushahidi wa Nassari, Lema
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema imeshindwa kuendelea na uchunguzi wa tuhuma za rushwa zilizowasilishwa na wabunge wa Chadema, Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) na Godbless Lema (Arusha Mjini).

Imesema uamuzi huo unatokana na wabunge hao kuingilia uchunguzi na kuuvuruga licha ya kutahadharishwa kuhusu suala hilo.

“Ni kweli tumeshindwa kuendelea na uchunguzi kwa sababu waliuingilia na kuuvuruga,” alisema Musa Misalaba, msemaji wa taasisi hiyo.

Hivi karibuni Nassari aliwasilisha Takukuru ushahidi mara tatu kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya madiwani waliojiuzulu kutoka chama hicho.

Madiwani hao walijiuzulu kwa kile walichoeleza kumuunga mkono Rais John Magufuli jambo ambalo Nassari anadai si kweli, bali walinunuliwa.

Katika ufafanuzi, Misalaba alisema wabunge hao waliingiza siasa katika uchunguzi huo, huku akitoa mfano wa kauli walizokuwa wakizitoa kwa waandishi wa habari kila walipokuwa wakiwasilisha ushahidi wao.

“Nadhani mnakumbuka wenyewe walivyokuwa wakifanya... taasisi iliona kama inaingizwa kwenye siasa. Sisi ni chombo huru kinachopaswa kufanya kazi bila kuingiliwa wala kushinikizwa na mtu,” alisisitiza.

Gazeti hili lilipomtafuta Lema jana saa mbili usiku alisema hana taarifa na kuahidi kuzitoa pale atakapozipata.

Oktoba 17, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Valentino Mlowola alimtahadharisha Nassari kuwa akiendelea kuingiza siasa kwenye suala hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Alisema kitendo cha mwanasiasa huyo kuweka hadharani taarifa za uchunguzi ni kinyume cha sheria kwa kuwa kazi hiyo inatakiwa kufanyika kwa siri na Mahakama ndiyo yenye jukumu la kuchukua hatua.

Alisema Takukuru ina wajibu wa kumlinda mtoa taarifa lakini jukumu hilo linakuwa tofauti kwa Nassari ambaye ameamua kujitokeza hadharani.

“Tulishampa angalizo kuwa mambo tunayoongea ni siri lakini mwenzetu inaonekana anafanya siasa kama anavyosema mwenyewe kuwa ataendelea kuleta ushahidi kama series ya Isidingo,” alisema Mlowola.

Wakati akiwasilisha ushahidi wake wa tatu Oktoba 16, Nassari alisema, “Huu ni ushahidi wa tatu na kwa kadri upelelezi ukiwa unaendelea nitaleta mwingine, hii ni kama filamu ya Isidingo.”

Nassari na Lema walifikisha malalamiko yao Takukuru kwa mara ya kwanza Oktoba 2 ikiwa ni siku moja kupita tangu walipouweka hadharani mbele ya waandishi wa habari ushahidi huo mjini Arusha.

Oktoba 4, Nassari alirudi tena Takukuru kwa lengo la kuwasilisha ushahidi na kuandika maelezo ya tuhuma zake kuhusu sakata hilo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search