Saturday, 23 December 2017

WANAJESHI FEKI WAWILI WAKAMATWA JIJINI DAR ES SALAAM

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kutumia sare za Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ) kufanya matukio mbali mbali ya kihalifu.


Wakati akizungumza na wanahabari jana Disemba 22, 2017 jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, SACP Lazaro Mambosasa, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Lainon Fratenus (20) na Noel Cleophace Wagesa (30) wote wakazi wa Kigogo.


“Jeshi la Polisi mnamo Disemba 15, 2017 majira ya saa sita usiku maeneo ya Lugalo Kawe polisi wakiwa dolia walifanikiwa kukamata wahalifu wawili wakiwa wamevalia sare za JWTZ na kisu kimoja huku wakitumia gari namba T 306 CRU Toyota Carina rangi ya fedha, wanatuhumiwa wanasadikiwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya uporaji jijini Dar es Salaam,” amesema.


SACP Mambosasa amesema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa ili kubaini mtandao mzima na matukio yote waliyowahi kufanya na baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa watapelekwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search