Friday, 12 January 2018

BINTI ALIYEPEWA UJAUZITO AKISOMA SEKONDARI ATUPWA JELA NKASI

Binti aitwaye Agatha Mwananyau (19) aliyekatiza masomo akiwa kidato cha nne baada ya kupewa ujauzito amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh 300,000/-.

Msichana huyo aliyekuwa akisoma kidato cha nne katika shule ya Sekondari Mkangale katika Mji wa Namanyere Wilayani Nkasi katika mkoa wa Rukwa aliacha masomo baada ya kupewa ujauzito na Alfa Nestory (20).

Jana aliitwa na upande wa mashtaka kutoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Nkasi mbele ya Hakimu Ramadhani Rugemalira ambapo alitoa ushahidi wa uongo akisema kuwa aliyempatia ujauzito hakuwa mshtakiwa Nestory bali alikuwa”mmachinga’ aliyetokea Mbeya tofauti na maelezo yake ya awali.

Kufuatia hali hiyo,ndipo Mwendesha Mashtaka , Hamimu Gwelo alipomshtaki kwa kutoa ushahidi wa uongo na aliposomewa mashtaka hayo alikiri kutenda kosa hilo.

Akitoa hukumu ,Hakimu Rugemalila alisema kuwa amezingatia utetezi wa mshtakiwa kuwa apunguziwe adhabu kwa kuwa ana mtoto mchanga mwenye umri wa miezi nane.

Mshtakiwa huyo alishindwa kulipa faini hiyo ambapo ameanza kutumikia adhabu hiyo.

Na Walter Mguluchuma- Malunde1 blog Nkasi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search