Monday, 15 January 2018

Dk Mashinji Aeleza Tofauti Yake na Dk Slaa

Dk Mashinji Aeleza Tofauti Yake na Dk Slaa


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amezungumzia madai ya kupwaya katika nafasi hiyo, akibainisha kuwa kila kiongozi ana mikakati yake katika utendaji wa kazi.

Akizungumza leo Januari 15, 2018 katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Televisheni ya Clouds, Mashinji amesema wapo wanaodai amepooza, mkimya na hana mikiki mikiki kama viongozi waliomtangulia walioshika nafasi hiyo.

Akitaja baadhi ya majukumu ambayo kwa sasa yanamtofautisha na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema, “Dk Slaa ilikuwa akizunguka mikoani, kuendesha mikutano, maandamano na harakati za matukio.

Katika uongozi wangu ninajenga  kanda za chama, kujenga uwezo wa chama ngazi za misingi(vitongoji).”

Amesema majukumu ya Katibu mkuu kwa sasa yamejikita katika utendaji wa kuimarisha mfumo, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa agenda ya chama hicho isemayo ‘Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli katika ujenzi wa Uchumi’.

“Sasa ukichanganya majukumu yangu na yale aliyokuwa akiyafanya Dk Slaa unaweza kuharibu mipango ya ujenzi wa kitaasisi. Watu  wanashindwa kuelewa hiyo tofauti, wanafikiria mfumo wa utendaji ni kama zamani,” amesema na kuongeza,

“Siyo kazi ndogo kujikita katika ujenzi wa kanda zetu inayotuelekeza kwenye Federal Government.”

Hata hivyo, amesema pamoja na mabadiliko hayo mazingira ya siasa kwa sasa nchini yamebadilika kutokana na hali ya ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na Serikali.

Amesema wakati Bob Makani (marehemu) alipokuwa Katibu Mkuu wa Chadema, majukumu yake yalikuwa ni ujenzi wa mfumo ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Amesemea baadhi ya kazi alizofanya tangu awe Katibu Mkuu ni  uandaaji wa Katiba ya Chadema, miongozo na kuweka misingi imara, mambo aliyodai kuwa yamemfanya asijulikane sana kwa Watanzania.

“Mbowe (Freeman-mwenyekiti wa Chadema) kwa wakati huo alikuwa maarufu kwenye umoja wa vijana. Makani hata leo wapo wasiojua kama alikuwa Katibu Mkuu wakati huo akiwa na mzee Mtei (Edwin-mwasisi wa Chadema),” amesema.

Dk Mashinji amesema kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, uongozi wa chama hicho  ulikuwa na kazi ya kukijengea umaarufu kupitia shughuli mbalimbali za matukio,  yakiwemo maandamano, mikutano ya hadhara na vikao.

“Kwa sasa kazi iliyopo ni ku- consolidate chama, kukijengea uwezo wa kitaasisi zaidi, kama ni umaarufu Chadema inajulikana, tunajaribu kuziba maeneo yaliyokuwa na pengo katika mabadiliko ya Katiba kwa mwaka 2006,”amesema.

Amesema chama hicho kinashindwa kufanya aina ya siasa kama ilivyokuwa wakati wa utawala uliopita kutokana na katazo la kufanyika kwa shughuli za siasa.

“Amsha amsha bado ipo, hata waliozuia wanajua hilo, anajua hata akitoa dakika mbili tu sasa hivi, hapakaliki, sasa wanazuia kwa kutokujiamini,” amesema

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search