Thursday, 25 January 2018

FOOLISH AGE.-SEHEMU YA KWANZA.JENNIFER ALPHONCE (0683777152)

WAKATI ULIOPO.
Asubuhi ya siku ya jumamosi ilikuwa na kibaridi na mawingu kiasi kuonesha kwamba kungekuwa na mvua wakati wowote ule katika mji wa Shinyanga.
Huku ndege wakizunguka huku na huko kufurahia siku mpya iliyokuwa imeingia.
Alfajiri ya saa kumi na mbili ilinikuta njiani nikitembea huku nikiwa na mawazo mengi.
Miaka kadhaa ya kuishi kwangu ilinibadilisha kutoka msichana mwenye thamani hadi kuwa mama asiye na mbele wala nyuma.
Nilitembea hali nikiwa na kipochi changu kidogo ambacho kilikuwa kimezoeleka sana kubebwa na wakina mama waliokuwa wakiuza mboga mboga.
Nilijifunga kitenge kikuu kuu ambacho hata rangi yake haikuweza kujulikana kwa kuwa kilikuwa kimechujuka sana na shati langu ambalo wakati nalinunua lilikuwa na rangi ya njano.
Mpaka wakati huo rangi yake ilikuwa inaelekea kwenye rangi ya maziwa.
Kichwani nilikuwa na nywele tano ambazo zilikuwa zimepauka na huku zimefumuka fumuka.
Miguuni nilikuwa nimevaa viatu vya wazi ambavyo navyo vilikuwa vimechoka sana.
Kila aliyeniona nadhani aliweza kujua kwamba ninapitia maisha magumu sana.
Nilitembea hatua za haraka haraka asubuhi hiyo huku nikijaribu kuwahi kufika kuikwepa mvua ambayo ilionekana kutaka kunyesha muda wowote ule.
Kutoka Ibinzamata nilitembea kwa hatua za haraka haraka na haikuchukua muda mrefu sana tofauti na ambavyo ingekuwa hadi kufika majengo mapya.
Nilianza kukata mitaa ya Majengo mapya na ndipo hofu ya moyo wangu ilipozidi kuongezeka, moyo ulikuwa ukipiga kwa kasi sana.
Ni miaka kumi sasa imepita niko Shinyanga hii hii lakini sijawahi kukanyaga huu mtaa.
Niliondoka kwa kebehi, kwa dharau na sasa ninarudi kinyonge sana.

Saa kumi na mbili hiyo watu wengi walikuwa bado hawajaamka.
Nilipishana na baadhi ya madereva daladala wachache waliokuwa wakiwahi shughuli zao zinazowapatia chakula cha kila siku.
Nilitembea kwa uwoga huku nikiwa na hofu kama ningewakuta wale ambao nilikuwa nikiwaendea asubuhi wakiwa tayari wameshaamka.
Na ghafla nilipaona mahali ambapo nilitaka kufika asubuhi hiyo.
Nyumba ilionekana kama mpya, ilikuwa nzuri sana iliyozungushiwa geti ambalo lilinakishiwa vizuri sana.
Nilisimama kwa muda huku nikitafakari kumbukumbu nyingi zilipita katika macho yangu.
Nilifumba macho huku nikijaribu kuzipoteza kumbukumbu hizo.
Machozi yalianza kunilenga kidogo kidogo.
Nilifungua upande wangu wa kanga na kisha kujifuta machozi yaliyokuwa yakianza kunianguka.
Na kisha nilipiga hatua za kichovu kuelekea kwenye geti hilo.
Nilipofika getini nilichungulia ndani ilionekana ni wazi kwamba bado hawajaamka wenyeji wangu.
Nilinyanyua mkono wangu nikiashiria kutaka kupiga hodi hata hivyo nilisita,

"Sijui nitakuwa nawasumbua." Nilijiuliza.
"Aanh ngoja tu nisubiri waamke."
Niliendelea kuwaza.
"Mmmh, sasa mvua ikinikuta hapa itakuwaje? Lakini ni sawa mie sitastahili kwanza sijui hata wameniitia nini."
Nilivuta ndala zangu na kisha kuzikalia pale pembezoni mwa geti.
Kadri muda ulivyokuwa ukizidi kujongea ndivyo upepo ulivyozidi kuongezeka na mawingu yalizidi kuwa meusi.
Mara nilisikia kilio cha mtoto mchanga akilia kutoka ndani ya hiyo nyumba.
Nilishituka.
"Mmmh!"
Nilinyanyuka kwa mshituko na kubaki nimekodolea macho ndala zangu pale chini kana kwamba zimefanya tukio la kustaajabisha.
Mawazo yaliyochanganyika na hofu yalinifanya nizidi kujikunyata pale mlangoni.
Hata hivyo nilisikia sauti ambayo kwa mbali nilihisi kuifahamu.
"Hello."
Niligeuka haraka haraka na kuchungulia kutoka pale pembezoni mwa geti.
Moyo ulinipiga paa..
Nilimfahamu mwanamke huyo.
Alipiga hatua za haraka na kisha kuja mlangoni kunifungulia.
Nilikuwa nimejikunyata huku mvua ikiwa imeshaanza kunyesha.

''Karibu ndani, kwanini hukugonga mlango?"
Aliongea kwa upole kama ambavyo alikuwa siku zote nilishindwa cha kujibu nilibaki nikimtazama kana kwamba ndiyo nakutana naye siku hiyo.
"Ingia ndani mama." Aliniongelesha kwa upole tofauti na nilivyotarajia.
Niliingia ndani na moja kwa moja nikaelekea kwenye veranda ili kujikinga na mvua ambayo ilikuwa ikizidi kuongeza kasi kadri muda ulivyozidi kwenda.
Sauti ya mtoto mchanga iliendelea kurindima humo ndani.
Nilijiuliza kama ikiwepo kuna mgeni amekuja.
"Karibu." Mara baada ya kufunga geti alinikaribisha ndani.
Niliingia mpaka sebuleni, kwa miaka kumi iliyopita sebule hiyo ilikuwa imebadilika sana ilizidi kuongezeka hadhi kana kwamba anaishi mfalme ndani ya nyumba hiyo.
Kulingana na maisha ambayo nilikuwa nikiishi mimi sehemu hiyo ilikuwa ni sehemu ya kifahari kuliko zote.
Nilipatazama kwa huzuni na uchungu sana.
"Ningekuwa nikiishi hapa mimi."
Niliongea na nafsi yangu.
Nilibaki tu nimesimama nikishangaa.
Kilichonivutia zaidi ni picha ya binti mzuri sana aliyekuwa akichekea kamera.
Nafsi iliniuma mpaka kufikia chozi kunidondoka.

"Karibu ukae." Aliongea.
Nilichagua kiti kilichokuwa pembeni yangu na kisha kukaa.
Mwanamke huyo alipita na kuelekea moja kwa moja mahali ambapo nilidhani ni chumbani kwake.
Rangi ya nyumba hiyo ilikuwa imebadilishwa.
Marumaru zake pia zilikuwa zimebadilika.
Na zaidi ya sana ziliongezwa marumaru nyingine ukutani.
Kulikuwa na vitu vingine vya thamani ambavyo vilikuwa vimeongezwa.
Hakika palikuwa panavutia sana.
Nilikaa nusu saa nzima nikiwa peke yangu huku nikiwa kama sijiamini.
Nilitamani kuita mtu lakini hata nilihisi kwamba sistaili, baada ya muda mrefu kidogo kupita mwanamama yule aliyenifungulia mlango alitoka akiwa amebeba mtoto.
Mtoto ambaye kwa kumkadiria alikuwa na kiasi kama cha miezi tisa.
Alikuja naye moja kwa moja mpaka nilipokuwa nimekaa na kisha akanikabidhi yule mtoto.
Nilikuwa nikitetemeka mwili mzima.
Nilimshika yule mtoto huku nikijaribu kumchekesha kwa namna yoyote niliyojua.
Mwanamke yule aliyenikabidhi mtoto aliondoka tena.
Nilisikia baadhi ya vitu vikigongana, mahali ambapo bila shaka nilipatambua kama jikoni.

Na baada ya muda alikuja kumchukua yule mtoto.
"Twende ukanywe chai."
Nilibaki tu nimetoa macho.
Wakati nimesimama huku nikiwa sijiamini kabisa kupiga hatua alitokea kipande cha mwanaume.
Pamoja na woga niliokuwa nao nilitembea kwa hatua za harakaharaka na kisha kupiga magoti mpaka chini na kumsalimia kwa kisukuma.
"Mwadela bhabha."
"Mwadela mayo."
Baada ya salamu hiyo nilinyanyuka.
"Za siku." Alinisalimia.
"Nzuri." Nikiongea huku nikikwepesha macho yangu kumtazama usoni.
Nilikuwa nikiangalia chini muda wote.
Mwanamama alidakia.
"Amenenepa, amekua mama sasa hivi."
Nilishindwa kugeuza macho uso wangu.
Nilitabasamu tabasamu lenye uchungu sana, huku nikitazama chini.
"Twende tukapate kifungua kinywa."
Tulielekea moja kwa moja mezani na kisha kupata kifungua kinywa.
Mwanamama yule alikuwa ameandaa vitu vingi sana kiasi kwamba sikuamini kama hivi vitu ni kwa ajili yangu au nimevikuta tu kwa bahati mbaya."
Baada ya matatizo yote, shida zote ambazo nilisababisha kwenye ile familia leo hii wana ujasiri wa kuniandalia chakula kizuri hicho.
Sikutaka kuamini kama ni maalumu kwa ajili yangu.
Nilikula kwa uwoga sana ingawa nilikuwa na njaa sana.
Ni muda mrefu sana umepita sijapata lishe ya kueleweka.
Baada ya kumaliza chakula hicho tulinyanyuka na kisha kuelekea sebuleni.
Nilijaribu kumsaidia yule mama kuondoa vyombo hata hivyo alinizuia.
Nilijua kabisa mahali hapo hapanihusu hivyo nitulie tu kama mgeni mara baada ya kusikia kitu ambacho nimeitiwa niondoke na kurudi tena kwenye kibanda umiza changu.
Baada ya kukaa peke yangu muda mrefu, hatimaye mwanamama yule na baba yule walikuja.
Safari hii walikuwa hawana mtoto mikononi mwao, walikaa.
Mwanaume yule alianza kwa kuvuta pumzi, nilizani angeanza kuongea na mimi hata hivyo alianza kuongea na mwanamama yule.
"Simuoni Tayo."
"Nimempigia simu lakini hapokei."

Walianza kujibizana wenyewe.
"Ngoja nijaribu tena."
Wakati mwanamama yule akihangaika kumtafuta Tayo, mwanaume yule alinigeukia mimi na kuanza kuniuliza maswali mbalimbali kuhusu hali niliyokuwa nikiishi.
"Maisha yanaendeleaje mwanangu?"
Nilimjibu tu kwa aibu.
"Yanaendelea vizuri."
"Kama yanaendelea vizuri basi tunashukuru."
Wakati huo mwanamke huyo alikuwa akihangaika kutafuta mawasiliano na Tayo aliweza kumpata.
"Hallo.... Tumekaa hapa tunakusubiri wewe mbona hufiki?
Hospitaliii...?!!!"
Kila mtu alishituka, hata mimi pia nilipatwa na woga.
"Hospitali gani? Kuna nini?"
Aliuliza maswali mfululizo.
"Sawa tunakuja sasa hivi."
Kumbukumbu ya matukio yaliyopita yalianza kupita kichwani kwangu.
Na hasa niliposikia Tayo yupo hospitali moyo ulinidunda kwa kasi.
Tulinyanyuka harakaharaka, tulijizoazoa na kisha kuelekea hospitali.
Nilipomuona Tayo moyo wangu ulishituka sana.


INAENDELEA.......

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search