Friday, 26 January 2018

FOOLISH AGE -SEHEMU YA PILI


JENNIFER ALPHONCE (0683777152)

Bila kupoteza muda tulikurupuka tukimbia kimbia huku mimi nikibaki tu nikikimbia pasipojulikana.
Nilifanikiwa kutoka hadi nje ya nyumba ile na kusimama getini.
Mwanamke yule ambaye alikuwa mama yangu mzazi alitoka nje akiwa amembeba mtoto na kufuatiwa na mwanaume yule ambaye alikuwa ni baba yangu mzazi.
Tuliingia kwenye gari la familia na kisha safari ya kuelekea hospitali ya mkoa ilipoanza.
Baada ya mwendo mfupi tulikuwa tumeshafika hospitalini hapo watu wengi walikuwa wakiongelea tukio hilo lililotokea, wakiongea kwa vikundi.
Mimi na familia yangu bado hatukuwa tukijua hasa ni kitu gani kilichokuwa kimetokea.
Tulipitiliza moja kwa moja mapokezi.
Mama alienda kuulizia pale mapokezini na kisha kuelekezwa.
Alitoka mbiombio huku na mimi nikimfungia tela hali nikiwa sijui chochote.

Kila mara picha ya Tayo ilinijia akilini kwangu.
Nilijikuta tu machozi yakinidondoka.
"Sijui atakuwa katika hali gani, sijui kama naye yupo kama mimi?"
Baada ya kukimbia kimbia kwa takribani dakika moja, hatimaye tulifika mahali ambapo Tayo alikuwepo.
Hakika hali yake haikuwa nzuri.
Mama alipomuona Tayo alianza kulia.
Aliangua kilio kikubwa sana.
Tayo aliponiona mimi na mama na baba naye alianza kulia.
Daktari alitutoa nje.
"Sasa nyie mmekuja kumfariji mgonjwa au mmekuja kumuongezea maumivu? Mtu kama yule anahitaji faraja kutoka kwenu lakini nyie mmekuja mnaanza kulia si mnamkatisha tamaa mwenzenu anahisi anaumwa sana ingawa hali yake siyo mbaya, hampaswi kulia mbele ya mgonjwa."
Daktari aliongea.
"Samahani dokta."
Mama alijibu.
Akili yangu haikuwepo hapo kabisa.
Ilinirudisha miaka kumi nyuma.

WAKATI ULIOPITA.


Katika familia yetu tulizaliwa watoto wawili tu mimi na Tayo.
Baba yangu aliitwa Samweli.
Baba yangu alikuwa akifanya kazi katika taasisi isiyokuwa ya kiserikali iliyokuwa ikijulikana kama Health Tanzania ambayo ilikuwa ikijishughulisha na maswala ya afya ya jamii.
Hivyo alikuwa akizunguka sehemu mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha huduma bora ya afya inatolewa katika vituo vya afya na katika maeneo ambayo huduma za afya zilikuwa hazipatikani.
Waliweka kambi kwa muda kutoa huduma kwa vile baba yangu alikuwa na taaluma ya udaktari.
Na pia walifanya takwimu ili kukusanya taarifa ambazo zingeisaidia serikali katika kutoa taarifa za kuhusiana na afya ya jamii kwa ujumla.
Mama yangu alikuwa ni mfanya biashara, yenye alikuwa msambazaji wa bidhaa za kampuni ya A.L.L ambayo ilikuwa ikijishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za usafi.
Kwa mfano dawa ya meno, sabuni za kuogea, za kufulia, dawa za kusafishia na vitu vingine kama hivyo.
Nilimzidi mdogo wangu Tayo kwa kiasi kama miaka mitatu na wakati huo mimi nilikuwa kidato cha kwanza Tayo alikuma yuko darasa la saba.
Kabla sijafika kidato cha kwanza mimi na Tayo tulikuwa tukisoma shule moja ya The Heavenlight Academy ambayo ilikuwa Kahama mjini na hata baada ya kumaliza elimu yangu ya msingi nilienda kujiunga na The Hollywood High School ambayo ilikuwa huko huko Kahama.
Mwaka wangu wa kwanza shuleni nikiwa kama kidato cha kwanza nilikuwa mzuri sana.
Shule yetu ilikuwa ni ya kifahari sana ambayo ilikuwa ikishindana na The Anderlake Ridges ilikuwa kama hoteli ya kifahari.
Wazazi wangu walilipa ada kubwa sana kwa sababu hawakupenda tuishi maisha ya shida.
Tulikula vizuri, tulikunywa tulichotaka, tulilala sehemu nzuri, mazingira yake yalikuwa ni mazuri sana.

Tulikuwa haturuhusiwi kutoka kabisa isipokuwa kwa jambo maalumu.
Wakati niko kidato cha kwanza nilipata marafiki wengi.
Shule yetu ilikuwa ni ya mchanganyiko.
Miongoni mwao walikuwa ni Christina, Janel, Dominic na wengineo wengi.
Nilifurahi sana kukutana nao.
Hata hivyo kati ya wote marafiki ambao walikuwa karibu nami zaidi walikuwa ni Christina na Janel.
Tulipendana sana hadi kutokea kuitwa mapacha watatu.
Kila sehemu tulifanya mambo yetu pamoja.
Mimi na Christina tulipangiwa chumba kimoja, vyumba vyetu vilikuwa ni vya watu wawili wawili.
Janel alikuwa akikaa kwenye chumba kingine na msichana mwingine ambaye alikuwa akiitwa Maria.
Kukaa kwetu chumba kimoja mimi na Christina kulizidisha mahusiano yetu.
Tulikuwa karibu zaidi na tulifanya vitu vingi pamoja.
Tuliambizana siri zetu za ndani, tukaambizana matatizo yetu na hata furaha zetu zilikuwa ni za pamoja.
Nilifurahi sana kupata rafiki mzuri kama Christina.
Christina alikuwa ni msichana mzuri sana.
Alikuwa na rangi nyeusi ya kuvutia, macho yake makubma na sura yake iliyopambwa na midomo mizuri kabisa.
Alikuwa na pua yake ndogo.
Alikuwa mrefu kunizidi na alikuwa na umbo zuri sana.
Kutokana na sifa zetu pale shuleni mapacha watatu tulikuwa wazuri sana na warembo kuliko wote shule nzima.
Kati ya wote mimi nilikuwa mrembo zaidi yao nilibarikiwa mwili ambao watu walizoea kuita umbo namba nane.
Sura nzuri, macho makubwa ya duara, vilipsi vyangu vidogo hakika viliupamba uso wangu.
Na zaidi ya yote sauti yangu nzuri ya kuvutia.
Walimu walinipenda sana kwa vile nilikuwa vizuri katika kuongea kingereza.
Na pia nilijitahidi sana katika masomo yangu.
Pamoja na yote hayo mapacha watatu tulikuwa tukifanya vizuri sana na kulikuwa na ushindani mkubwa katikati yetu.
Maisha yangu wakati nipo kidato cha kwanza yalinifanya niwe maarufu sana pale shuleni.
Tulijulikana hadi kwa kidato cha sita.
Kila wadada wa kidato cha sita walipenda tuwe wadogo wao.
Tulikuwa gumzo vinywani mwa kila mwanafunzi Hollwood High School.
"Yani hapa shuleni kuna warembo wengi lakini Naomi, Christina na Janel wamewazidi wote, hawa watoto ni very hot."
Ni mazungumzo ya kila siku yaliyokuwa yakisikika hapo shuleni.
Hata hivyo hatukujali, tulipendelea sana kusoma.
Mara nyingi sana Janel alikuwa akitumia muda wake mwingi kukaa kwenye chumba chetu.

Alikuja, tulipiga stori mpaka muda wa kwenda kulala mara baada ya kutoka prepo na siku za mwishoni mwa wiki alikuwa akikaa chumbani kwetu muda wote.
Siku nyingine alilala kabisa ingawa matroni alikuwa akizuia sana kulala kwenye vyumba ambavyo sio vya kwetu lakini kiubishi ubishi tu alilala.
Alipoamka asubuhi, Janel alikuja kwetu kuanza kutuamsha.
"Amkeni nyie mnapenda sana kulala."
"Aanh wewe asubuhi asubuhi yote hii unaenda kufagia madarasa? Au leo zamu yako?"
"Aanh amna bwana amkeni tujiandae."
Janel alipenda sana kuamka mapema ingawa alikuwa anapenda sana kulala.
Kati ya wote mimi nilikuwa nikiongoza kwa kulala, nilipenda sana.
Muda wangu wa usiku niliutumia kusoma.
Christina alipenda sana kulala hata hivyo alikuwa akiamka usiku wa manane kusoma, alisema huo muda ndiyo ambao anaelewa vizuri.
Sikuweza kumpinga kama ni muda wake ambao alikuwa anasoma na kuelewa nilimuacha awe huru kwa ajili ya matokeo mazuri kwetu wote.
Ilikuwa ni sheria yetu mtu anaposoma hakuna kumsumbua.
Mimi na Christina tulikuwa ni waromani katoliki wakati Janel alikuwa ni mlutheri ambaye yeye alikuwa akisali katitika Umoja wa Wanafunzi wa Kikristo Tanzania. (UKWATA.)
Walimu walitupenda sana.
Na pia tulifanya vyema katika masomo yetu.
Katika tatu bora tulikuwa tukibadilishana tu namba, hii ilifanya walimu wazidi kutupenda.
Hata hivyo ilifanya shetani pia azidi kutupenda.
Nilienda nyumbani wakati wa likizo baada ya kumaliza kidato cha kwanza.
Mdogo wangu Tayo naye alitaka kuja kusoma shuleni kwetu hasa baada ya kusikia sifa za shule yetu.
"Na mimi nataka kwenda kusoma Hollywood na dada."

"Mimi nilikuwa nataka nikusomeshe shule ya tofauti."
Mama yangu alisema.
"Hapana mimi nataka kwenda kusoma huko huko."
"Sawa kama unataka mtaenda wote."
Hatua za mwanzo kabisa za kumpatia nafasi katika shule yetu zilikamilika.
Likizo yangu ilikuwa nzuri sana kwani tulienda kutembea maeneo mengi ya burudani tulijifunza mambo mengi.
Ingawa kwetu haikuruhusiwa kutoka bila kuwa na uangalizi maalumu nilijihisi kama mfungwa.
Shuleni nabanwa, nyumbani nabanwa.
Hata hivyo kwangu ilikuwa kawaida sana.
Baada ya likizo tulirejea shuleni nikiwa nimeongozana na Tayo.
Mwaka huo ulikuwa wa tofauti sana sio kama uliopita.
Kila kitu kilichokuwepo kilibadilika.


INAENDELEA.........

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search