Wednesday, 3 January 2018

Jini Kabula Asimulia Matatizo Yake ya Ugonjwa

Maskini Jini Kabula Asimulia Matatizo Yake ya Ugonjwa 'Nilikuwa Kuzimu Sasa Nimerudi'
                                                                                                                                                                    MIRIAM Nyafulwa Jolwa ‘Jini Kabula’, msanii aliyekumbana na janga kubwa la kuugua ugonjwa uliotajwa kama ‘kichaa’ kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, ameibuka na kufunguka kuwa kwa mapito aliyopitia mwaka 2017 anaona ni kama alikuwa kuzimu kisha kurejea duniani.Pamoja na hilo, Jini Kabula amefungukia mengine mengi likiwemo suala la kudaiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Jini alizungumza hayo, baada ya mwanahabari wetu kumpigia simu kwa lengo la kumjulia hali na kutaka kujua kwa namna alivyojiandaa kuukaribisha mwaka mpya 2018, mazungumzo yalikuwa hivi:

Risasi Mchanganyiko: Jini vipi hali yako kwa sasa? Umepona kabisa?

Jini Kabula: Kabisa, si unaona tunaongea vizuri tu! Niko salama kabisa.

Risasi Mchanganyiko: Kwani ulikuwa unaumwa nini hasa?

Jini Kabula: (kimya cha muda mfupi), ndugu yangu wewe acha tu ni mapito ya duniani. Nashindwa kubainisha moja kwa moja nilichokuwa naumwa lakini nikiri ukweli kwamba sikuwa sawa kiakiki na kimwili, nilikuwa dunia ya peke yangu na ndiyo maana namshkuru sana Mungu kwa kunitoa jehanamu, maana ni sawa na nilikuwa kuzimu, ndiyo maana kwa sasa napumzika na hata hii simu nimepokea kwa sababu ni wewe, naongea na ndugu zangu tu.

Risasi Mchanganyiko: Kwani kwa sasa uko wapi?

Jini Kabula: Niko Mwanza kwa kaka yangu, niko mapumzikoni. Nauweka mwili wangu sawa kabla sijaanza tena mapambano ya maisha.

Risasi Mchanganyiko: Nini kilikuwa chanzo cha tatizo lako?

Jini Kabula: Tutazungumza tukikutana ana kwa ana lakini kwa sasa niseme tu kwamba kuugua kwa binadamu ni kawaida lakini wao walifurahi lakini Mungu ametenda na nitamtumikia hadi mwisho wa maisha yangu.

Risasi Mchanganyiko: Akina nani unaowasema walifurahi na Mungu ametenda?

Jini Kabula: (akilitaja jina la mwandishi) nimesema tutazungumza tukionana ana kwa ana lakini kwa sasa niseme watu wana visa sana.

Risasi Mchanganyiko: Kwa sasa umepona, kuna ndugu na marafiki waliokutenga wakati unaumwa? Kama wapo utachukua uamuzi gani?

Jini Kabula: Ni kweli kuna waliokuwa mbali na mimi lakini ni kawaida sana. Unajua mtu anapoumwa hususan ugonjwa wangu ule, ni vigumu watu kuwa karibu lakini ninawashukuru baadhi ya wasanii waliopambana kuokoa maisha yangu, hususan dada yangu Esha Buheti, Mungu ambariki sana na hakika maisha yake yamebarikiwa, ni mwanamke mwenye roho ya utu na uungwana uliopitiliza.

Risasi Mchanganyiko: Wakati unaugua kuna madai yalienea kwamba ulipimwa na kugundulika una Virusi vya Ukimwi, hili likoje?

Jini Kabula: Walisema hivyo? Jamani lakini nashukuru. Mimi ni mzima wa afya kabisa. Sina Ukimwi, tukionana nitakwenda kupima mbele yako.

Risasi Mchanganyiko: Umefikiria kuolewa sasa? Ni aina gani ya mwanaume unayemtaka?

Jini Kabula: Kuolewa? Lazima lakini siyo sasa hivi.

Risasi Mchanganyiko: Umeachana na maisha ya anasa? Kama pombe na starehe zingine?

Jini Kabula: Hapana kabisa. Mimi ni mtu wa Mungu na nimebadili mfumo wa maisha yangu, siwezi tena kufanya upuuzi huo.
Chanzo: Global Publishers

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search