Thursday, 11 January 2018

Kubenea: Lowassa ameonesha njia

Saed Kubenea

HATUA ya Edward Lowassa, waziri mkuu mstaafu na mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2015 ya kukutana na Rais John Magufuli, imezusha taharuki ndani na nje ya chama chake.

Kinacholeta taharuki, ni kauli zake kuhusiana na utawala wa Magufuli. Binafsi, nimewasikiliza wote.

Hata hivyo, naomba niseme machache.
Kati ya mwaka 1995 hadi 2010, Zanzibar ilikumbwa na mkwamo mkubwa wa kisiasa.

Ndani ya visiwa hivyo, uhasama ulitalamaki. Fitina na maonevu mengine lukuki - yalikuwa yameshamiri.

Jemedari la kisiasa Visiwani, Maalim Seif Sharif Hamad, aliamua kukutana na hasimu wake mkuu kisiasa, Rais Amani Abeid Karume.

Mkutano kati ya Seif na Karume, ulifanyika wakati mamia ya wananchi wa Pemba wakiwa ukimbizini nje ya nchi.

Aidha, wakati Maalim anakutana na Karume, makumi ya akina mama walikuwa wamebakwa na kulawitiwa na watu wengine kadhaa walikuwa wamefunguliwa kesi za jinai mahakamani.

Si hivyo tu: Mamia ya wananchi, hasa wafuasi wa CUF walikuwa wamefutwa kazi serikalini.

Wengine kadhaa, wakiharibiwa mali zao, yakiwamo majumba, mashamba na baadhi wakiwa wameachwa wajane kutokana na mateso waliyopata wenza wao.

Maalim alikutana na Karume kimya kimya na bila kushirikisha wenzake kwenye chama.

Alikutana na kuzungumza na Karume na kukataa katakata kutaja kile walichojaliana.

Ilidaiwa kuwa Maalim alichukua hatua hiyo kwa kuwa alihofia kuwa kueleza mapema kile walichojadili; na au wanachokwenda kujadiliana, kungevuruga mikakati yake.

Hata Rais Karume naye hakueleza kuwapo mkutano na Maalim Seif. Hakueleza walichotaka kukizungumza na wala hakusema kile walichokijadili baada ya mkutano wao.

Mkutano kati ya viongozi hawa wawili ulifanyika wakati tayari vyama vya CUF na CCM, vikiwa vimefunga miafaka mitatu ya kisiasa bila mavuno kwa CUF.

Mwasisi wa mazungumzo kati ya Karume na Seif, ni mzee Nassoro Moyo, Eddy Lyami na Mansour Hamid.

Baada ya taarifa za kuwapo mkutano huo kuvuja, wafuasi wa CUF walikuja juu. Walimtukana Maalim Seif matusi ya nguoni.

Nakumbuka katika mkutano mmoja wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti, wafusi wa chama hicho, walimtupia mawe na maganda ya machungwa kiongozi wao huyo.

Kuna mengi ya kueleza juu ya tukio hilo. Lakini itoshe tu kusema, mkutano kati ya Maalim na Karume ndio uliozaa Katiba mpya ya Zanzibar na ndio msingi wa CUF kuingia serikalini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Hivyo basi, naifananisha ziara ya Lowassa ya jana na tukio hilo la mwaka 2010 Visiwani.

Lowassa amekutana na Magufuli, kipindi ambacho chama chake kiko kwenye mkwamo. Hakiwezi kufanya mkutano wa hadhara.

Kimefika mbali zaidi; sasa hata uchaguzi mdogo hakiwezi kushiriki.

Baadhi ya viongozi wakuu chama badala ya kuwaongoza wanachama, nao wamegeuka kuwa walalamishi.

Ni kwa sababu, CHADEMA ya mwaka 2010 hadi 2014 ya maandamano na mikutano haipo tena.

Katika muktadha huo, njia pekee ya kutoka hapa tulipo ni kujadiliana adui yako. Lowassa amefungua njia hiyo. Ni vema ikatumiwa.

Mwisho

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search