Tuesday, 2 January 2018

MBOWE ASHANGAZWA NA WABUNGE NA MADIWANI WALIOHAMA KUMUUNGA MKONO MAGUFULI


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amewashangaa viongozi na wanachama wa chama hicho wanaohama na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa madai kwamba wanamuunga mkono Rais, na kusema haoni sababu ya viongozi hao kuipongeza serikali.


Mbowe ameyasema hayo leo Disemba 31, 2017 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu matukio mbalimbali yanayoendelea nchini na kusema kuwa watu wanakufa hovyo, vyuma vimekaza, hivyo anawashangaa wanaosema kwamba wanaiunga mkono serikali.


Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai ametoa mifano kadhaa akionyesha matendo ambayo serikali hii inayetenda na kusema kwa kiongozi mwenye akili timamu hawezi kuhama na kuunga mkono serikali.


“Ni bora basi wanaohama wakatoa na sababu nyingine yenye akili. Mnapohama wote na wimbo mmoja kama kasuku, inatufanya tujiulize kwanini hawa wote wanaohama wanafurahia tu bwana mkubwa anapiga vita ufisadi?”


“Aliyesema ajenda za siasa ni ufisadi peke yake ni nani? Uchumi unaporomoka, vyuma vimekaza nchi nzima, wewe unampongeza Rais kwa lipi? Vyombo vya habari vinafungiwa, wewe unampongeza Rais kwa lipi? Miili ya watu waliouawa inaokotwa inaelea bahari, wewe unaipongeza serikali kwa lipi? Wewe Mbunge na Diwani mwenye akili timamu unaipongeza serikali wakati Lissu ana majeraha ya risasi 16?” alihoji Mbowe.


Mbowe amesema kwamba, wanasiasa waliohama kwa sababu hizo, wanawatakia kila la heri na kwamba wanaamini wataifika salama kwa sababu walipokuwa hawakuwa sehemu sahihi.


Mbowe ameeleza kwamba, kama wanaohama wangekuwa wanatoa sababu mbalimbali, mfano mwingine aseme uchumi upo vizuri, kilimo kimewekewa mikakati madhubuti au ajira na mishahara imeongezwa, ingekuwa afadhali kuliko kumsifia bwana mmoja ambaye nchi nzima inaugulia kwa sababu yake.“Ili mti ukue, lazima majani ya zamani yapukutike, ili mengine mapya yachipue,” alisema Mbowe.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search