Wednesday, 10 January 2018

MBOWE SIKUMTUMA LOWASA KWA MAGUFULI


Baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa kumtembelea Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya nae mazungumzo, Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe amekanusha kuwa kile kilichosemwa na Lowassa hakitokana na msimamo wao.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji BBC, Mbowe alisema wao kama Chama wamekuwa na utaratibu wa kutoa msimamo wao na kueleza kuwa kwa siku za hivi karibuni wamekuwa na malalamiko dhidi ya Rais na Serikali yake kuhusu kuminywa kwa Uhuru wa Bunge, Mahakama na kuminya Demokrasia.

" Tunaona jinsi ambavyo uhuru wa watu unaminywa, uhuru wa vyombo vya habari, wandishi, wanasiasa na wananchi kutekwa, kudorora kwa uchumi, unaanzaje kumuunga mkono Rais nafikiri muhusika aulizwe mwenyewe," alisema Mbowe.

Kuhusu kauli ya Lowassa kusifia ongezeko la ajira, Mbowe anasema hayupo tayari kujibu hoja hiyo lakini akaeleza namna ambavyo makampuni mengi yanafungwa hivi sasa, kundi kubwa la vijana wasio na ajira likiwa mitaani.

" Nisikitike tu kuwa sisi tuna tatizo kubwa sana la kumuuguza Lissu ambaye alipigwa na risasi, kweli anaweza kutoka kiongozi mkubwa na kumsifia Magufuli wakati tunauguza watu? Msaidizi wangu Ben Saanane amepotea hadi leo, wabunge wetu wanafukuzwa bungeni hivyo niseme tu hakuna msimamo kama huo ndani ya Chama labda atafutwe muhusika mwenyewe aeleze," Alisema Mbowe.

Akizungumzia hama hama kwa wabunge na wanachama wa upinzani na kujiunga na CCM sambamba na tukio la leo la Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama hicho, Muslim Hassanal kujiunga na CCM leo, Mbowe alisema suala la wapinzani kuhamia CCM halijaanza leo na kwamba suala la kujenga upinzani ulio imara lazima lipitie hatua mbalimbali ili kufanya mchujo wa kubakia na watu wenye dhamira ya kweli.

NUKU YA MBOWE KUHUSU SUALA LA LOWASA KWENDA IKULU
Kauli iliyotolewa na Mhe. Lowassa katika ziara yake ya Ikulu jana, Kwa alichokizungumza pale ule sio msimamo wa Chama, Sisi kama Chama tunafanya maamuzi kupitia vikao, na tunatoa maazimio ya pamoja, baada ya kutafakari na kujadiliana kwa upana wake kuhusu jambo lenyewe.

Katika siku za karibuni tumekuwa na malalamiko mengi sana dhidi ya Rais na Serikali yake, tumeona namna ambavyo Rais anaminya demokrasia katika Taifa, tumeona namna ambavyo Rais ananyima uhuru wa Bunge, tunaona namna ambavyo Rais ananyima hata uhuru wa mahakama, tunaona jinsi tume ya uchaguzi na vyombo vya ulinzi vinavyosaidia kuchafua uchaguzi,kuchafua chaguzi mbalimbali za marudio.

Tunaona jinsi zoezi haramu kujaribu kuwarubuni viongozi mbalimbali hasa wawakilishi wa wananchi hasa wa Upinzani linavyofanyika.

Tunaona uchumi wa nchi unadidimia,waandishi wa habari wanapotezwa, uhuru wa vyombo vya habari unazidi kupotea,uhuru wa watu kutoa mawazo unazidi kudidimia katika mazingira hayo ya uchumi kumomonyoka na maisha ya watu kuzidi kuwa magumu tunashindwa kujua unapata wapi ujasiri wowote ule wa kuweza kusifu Serikali ya awamu ya tano ambayo ni ya Rais Magufuli, huo sio msimamo wetu wa Chama.

Siyasemi haya kubishana na kauli alizozitoa Mhe. Lowassa, pengine yeye anazo takwimu zake tofauti ambazo tunazijua kwa sababu amezungumzia kuhusu ajira lakini hakusema kutolewa kwa ajira ngapi? Japo imelinganishwa na ujenzi wa reli ya kati unaweza ukaongeza ajira, Naona kuna tatizo kubwa la ajira katika nchi, na kuna ongezeko kubwa la vijana wengi ambao hawana ajira,tunatambua wanamaliza Shule hawapati ajira, lakini vile vile kuna makampuni yanafungwa,biashara zinafungwa, benki zinaelekea kufungwa nafasi nyingi za ajira zinapotea.
Na sio kila tamko linalotolewa na mwanachama au kiongozi wa CHADEMA mahali popote ni tamko rasmi la Chama, nisikitike tu kwamba sisi tuna kilio kikubwa,utakumbuka kwamba tunaendelea kumtibu Mhe. Tundu Lissu ambae alishambuliwa kwa risasi, unashindwa kupata ujasiri wowote, unashindwa kupata ujasiri wowote, kiongozi wa CHADEMA kweli unamsifia Magufuli, wakati tunauguza watu, msaidizi wangu Ben Sanane amepotea, viongozi wetu wameuawa, wengine wamefungwa, Wabunge wanafukuzwa Bungeni, wakina Ester Bulaya, Halima Mdee kwa mashtaka ambayo ni ya kubambikiza ambayo hayafuati kanuni za Bunge.

Mimi kama kiongozi Mkuu wa chama nasema huo sio msimamo wa CHADEMA.

Kuhama watu kutoka chama kimoja kwenda chama kingine, haijawa jambo geni kwenye siasa za Tanzania, kazi ya kujenga Upinzani katika Taifa letu sio tukio la siku moja ni mchakato wa muda mrefu, lazima ipitie vipindi mbalimbali ambapo linafanya mchujo wa asili na kubakiza watu wachache ambao watasonga mbele wataleta uhuru wa kweli Maendeleo ya kweli na haki zote za kidemokrasia katika Taifa.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search