Monday, 29 January 2018

Mbunge Upendo Peneza kuwasilisha hoja binafsi Serikali itoe taulo za hedhi kwa wanafunzi

Image result for UPENDO PENEZA
Dar es Salaam. Mbunge wa viti maalum (Chadema), Upendo Peneza anatarajia kuwasilisha hoja binafsi kwenye mkutano wa Bunge kuiomba Serikali kutoa bure kwa wanafunzi taulo za kujihifadhi wanawake wakati wa hedhi.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 29, 2018, Peneza amesema tayari ameiwasilisha hoja yake Ofisi ya Spika wa Bunge kwa ajili ya hatua zaidi.

Amesema haiwezekani mtoto wa kike akakosa mwezi mmoja na siku 12 za masomo kwa mwaka wakati Serikali inaweza kuzigharamia taulo hizo kwa kununua na kuzigawa bure.

“Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, ukitaka kuwasilisha hoja binafsi unaandika barua kwa Spika jambo ambalo nimelifanya. Desemba mwaka jana na Januari 5 mwaka huu nilijibiwa kuwa naweza kuendelea,” amesema Peneza na kuongeza,

“Ukijibiwa kanuni inakutaka kuwasilisha hoja hiyo kwa Spika siku moja kabla ya mkutano kuanza. Mkutano wa kumi wa Bunge la kumi na moja unaanza kesho. Hoja yangu niliiwasilisha wiki moja zaidi ili kutoa fursa kwa uongozi wa Bunge kuiangalia. Naamini nitapewa fursa ya kuiwasilisha.”

Peneza amesema suala hilo linahitaji ushirikiano wa wabunge wote na jamii nzima bila kujali itikadi za vyama ili kuwawezesha watoto wa kike kusoma kwa furaha wakati wote.

“Wanapokuwa katika kipindi cha hedhi wanaweza kushawishiwa na wanaume kuwa watawanunulia taulo za kike, hatutaki watoto wetu wakose amani, furaha au kushindwa kuhudhuria masomo. Serikali wakati ikijikita kutoa elimu bure iangalie na suala hili ambalo ni muhimu sana,” amesema.

Peneza amesema tayari ameshazungumza na uongozi wa wanawake wabunge ili atakapowasilisha bungeni wawe na uwelewa huku akiwaomba wabunge wanaume kumuunga mkono katika harakati zake za kumtetea mtoto wa kike.


Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search