Thursday, 25 January 2018

MWALIMU AUAWA KWA KUPIGWA NA WAFUGAJI AKIDHANIWA NI JAMBAZI


Picha haihusiani na habari hapa chini
Watu watatu akiwamo mwalimu wa shule ya msingi mjini Korogwe mkoani Tanga wameuawa kwa kushambuliwa na wafugaji waliokuwa wakijihami kutokana na tukio la ujambazi lililotokea katika maboma yao Jumamosi iliyopita.Watu hao waliuawa kwa silaha za jadi baada ya kufika katika kijiji cha Mswaha darajani wilayani hapa saa 8:00 usiku wakiwa na gari ndogo ambayo haikuwa na namba za usajili wakitafuta mkaa.


Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema mauaji hayo yalitokea kijiji cha Mswaha Darajani wilayani hapa.


Aliwataja waliouawa kuwa ni Omar Mhina (38) ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Nzugunati aliyekuwa akiendesha gari hiyo baada ya kupotea njia ya mahala walipokuwa wakielekea, walitokea kwenye maboma ya wafugaji.


Wengine waliouawa ni Ismail Bakari na mbebaji wa mkaa ambaye hadi jana alikuwa hajafahamika jina, ambao awali walikuwa wamekimbia eneo alilokuwa akishambuliwa mwalimu Omar na kujificha porini ambako walikutwa baada ya wafugaji hao kufanya msako mkali.


Bukombe alisema chanzo cha mauaji hayo ni tukio la uporaji wa kutumia silaha aina ya gobore, mfugaji mmoja kijijini hapo Loyshiru Nyangnyi (48) alivamiwa nyumbani kwake na kuporwa pikipiki aina ya SunLG na Sh2.5 milioni kisha kujeruhiwa kichwani kwa risasi.


Alisema kufuatia mauaji hayo, watu wanne wanashikiliwa kwa kosa la kujichukulia sheria mikononi, badala ya kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria. 

Na Burhani Yakub, Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search