Wednesday, 24 January 2018

Mwanakwaya afariki Dunia baada ya kutoa sadaka

Mwanakwaya wa kwaya ya Mtakatifu Secilia, Kigango cha Muze Parokia ya Zimba, Jimbo Katoliki Sumbawanga, Flora Nandi (25) ameanguka na kufariki dunia muda mfupi baada ya kutoa sadaka ya shukrani akiwa kanisani.

Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita saa nne za asubuhi wakati wa ibada ya kwanza wakati kwaya ya Mtakatifu Secilia ilipokuwa ikimsifu Mungu katika ibada hiyo.

Akizungumzia tukio hilo, mwalimu wa kanisa aliyekuwa akiongoza ibada hiyo, Katekista Philipo Lupadasi alisema wanakwaya wakiwa wanaimba na marehemu akiwa ametoka kutoa sadaka ya shukrani alirejea katika sehemu yake kwenye kwaya na kuendelea kuimba lakini ghafla alianguka chini hali iliyozua mshtuko na kusababisha ibada kusimama kwa muda.

Alisema wanakwaya wenzake walimnyanyua na kumtoa nje ya kanisa ili apate hewa wakiamini kuwa amepoteza fahamu. Katekista huyo alisema baada ya kumpepea kwa muda, waliona hapati fahamu hali iliyowalazimu kumpeleka Zahanati ya Kijiji cha Muze kwa ajili ya matibabu.

Alisema baada ya kufikishwa katika zahanati hiyo alipokewa na wahudumu wa afya ambao baada ya kumfanyia uchunguzi walibaini kuwa alikuwa ameshafariki dunia.

Baada ya kupewa taarifa za kifo hicho, wanakwaya hao waliangua kilio na hawakuweza kurudi tena kanisani kuimba katika ibada ya pili na badala yake waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka nyumbani kwake kwa taratibu za mazishi.

Mwalimu wa kwaya hiyo, Aloyce Mwandanje alisema kuwa kifo cha mwanakwaya mwenzao ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi mitano, kimewaachia majonzi makubwa lakini hawana la kufanya kwa kuwa ni mapenzi ya Mungu.

Alisema mwili wa marehemu Nandi ulizikwa Jumatatu katika makaburi ya Kijiji cha Muze.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search