Tuesday, 2 January 2018

NAPE APONDA WANASIASA WANAO HAMAHAMA VYAMA

Related image
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amehoji sababu za vyama vya siasa kuhangaika kupokea wanachama wa vyama vingine, badala ya kushughulika na Watanzania wasio na vyama.


Akizungumza leo Jumapili Desemba 31,2017 katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam, Nape amesema siku zote amekuwa na msimamo tofauti na wanachama wanaovihama vyama vyao kwa maelezo kuwa unawajenga wanaohama, si vyama.


"Kama tunataka kujenga vyama viwe vya kitaasisi ni lazima kuhamahama lisiwe suala la kawaida. Yaani mtu mpaka anahama watu waseme kweli huyu alistahili kuhama," amesema Nape.


Amesema, "Watanzania wapo zaidi ya 50 milioni, wenye uwezo wa kujiunga na vyama kikatiba wanaweza kuwa zaidi ya 30 milioni, waliopo kwenye vyama wanaweza wasifike 10 milioni. Kwa nini tunakwenda kuhangaika na wanachama wa vyama vingine badala ya kushughulika na Watanzania wasio na vyama. Tushughulike kuwashawishi hawa."


Katika kipindi hicho, mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro na mwanahabari mkongwe, Dk Gideon Shoo waliungana na Nape kukosoa vitendo vya wanachama kuvihama vyama vyao.


Kwa mtazamo wao, hamahama ya wanasiasa ni miongoni mwa kasoro zilizojitokeza mwaka 2017.

Na Fidelis Butahe, Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search