Monday, 22 January 2018

SERIKALI YAZIFUTIA USAJILI MELI 2 ZILIZONASWA NA DAWA ZA KULEVYASERIKALI imezifutia usajili meli mbili zilizokamatwa kwa kupakia shehena za dawa za kulevya na silaha kinyume cha sharia, huku zikiwa zinapeperusha bendera ya Tanzania.

 Aidha imesema itaanzisha utaratibu wa kuzifanyia uchunguzi wa kina meli zote mpya zitakazoomba usajili pamoja na wamiliki wake kwa kushirikisha vyombombalimbali vya serikali, vikiwemo vile vya ulinzi na usalama ili kuondokana na utata na dosari zinazoharibu sifa njema ya nchi.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa maazimio ya mkutano kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushughulikia meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania kwa tuhuma za kusafirisha silaha na dawa za kulevya.

Alizitaja meli hizo zilizokamatwa kuwa ni Kaluba yenye usajili namba IMO 6828753 iliyokamatwa Desemba 27, 2017 ikiwa na wastani wa kilo 1,600 za dawa za kulevya huko katika maeneo ya Jamhuri ya Dominica. 

Meli nyingine ni Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa kwa kusafirisha silaha kinyume na Sheria za kimataifa kwenda Libya na zote mbili zimesajiliwa Tanzania kupitia Taasisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya kusajili meli za nje.

Alisema: “Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Vita Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya na pia ni Mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Vita Usafirishaji Haramu wa Silaha. Hivyo Tanzania imejidhatiti na imedhamiria kutekeleza majukumu yake yaliyoelezwa katika mikataba hiyo ya kimataifa”.

Alisema moja ya majukumu hayo ni pamoja na kushirikiana na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa katika kupiga vita usafirishaji wa dawa za kulevya na silaha. 

Alisema: “Taarifa ya kukamatwa kwa meli zenye bendera ya Tanzania zikisafirisha dawa za kulevya na silaha ni kinyume na Sheria za nchi yetu na zile za kimataifa. Taarifa hizi zimeleta mshtuko mkubwa ndani ya nchi yetu, hasa kwa kuwa Tanzania imejipambanua kupambana na maovu hayo kwa kutumia nguvu zote”.

Samia alisema kutokana na taarifa hizo, Rais alimuagiza kuitisha kikao cha dharura baina ya viongozi na wataalamu wa pande hizo mbili kuzungumzia kadhia hiyo ambapo kikao hicho kilifanyika juzi Zanzibar na kuhudhuriwa pia na Balozi Seif Ali Idi, Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar. Alisema kikao hicho kilibaini kwamba suala la usajili wa meli za nje linafanywa na nchi nyingi duniani na kwamba wenye meli hupendelea kusajili meli zao nje ya nchi zao kwa kukimbia uzito wa kodi na sheria zinazobana shughuli zao.

Alisema kutokana na hilo wameamua kutoa taarifa hiyo kwa Tanzania na dunia kwa ujumla ili kuondoa upotoshaji wa aina yoyote kwa kupitia vyanzo visivyo rasmi. Aidha, alisema wanazifanyia mapitio sheria ili kuzipa nguvu zaidi taasisi zinazosimamia usajili wa meli ambapo wakati wa mapitio ya sheria, timu ya wataalamu itaangalia kwa makini kodi zinazotozwa na mchango wake nchini ili zisiwe kivutio kwa meli zisizokidhi viwango kuomba usajili Tanzania.

Alisema kwa mujibu wa mkataba wa UNCLOS 1982 kila nchi imepewa haki ya kufanya usajili wa meli kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa na sheria za nchi husika na kwa upande wa Tanzania, usajili wa meli za kimataifa unasimamiwa na Sheria Na 5 ya mwaka 2006. Alisema kwa upande wa sheria ya Sumatra ya meli ya mwaka 2003 inaruhusu usajili wa meli inayomilikiwa na Mtanzania, au meli inayomilikiwa kwa ubia kati ya Mtanzania na raia wa nchi nyingine.

Pia alisema kampuni hiyo ya umiliki lazima iwe ya Kitanzania kwa maana ya kusajiliwa na kujiendesha kutokea Tanzania hata kama kampuni hiyo inamilikiwa na watu wasio Watanzania. Kwa upande wa Zanzibar kupitia ZMA wana sheria ya mwaka 2006 ambayo inaruhusu usajili wa meli yoyote hata kama mmiliki wake sio Mtanzania wala kampuni kuwa ya Kitanzania hivyo kutoa fursa kwa meli ambayo haina umiliki wa aina yoyote wa Tanzania kwa maana umiliki na ukazi kupewa usajili wa kupeperusha bendera ya Tanzania nje ya Tanzania.

Aidha alisema sheria hizo huendeshwa sambamba pamoja na Sheria na Kanuni za Kimataifa, hivyo Sheria na Kanuni hizo humlazimu mwenye meli, kujaza fomu maalumu ya maombi pamoja na fomu zingine na ndipo hatua nyingine za kufanya uchunguzi wa historia ya meli kupitia vyanzo mbalimbali tangu meli ilipotengenezwa hadi muda inapoomba usajili.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya 1988 na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa 1970 (2011), nchi zilizosajili meli zinazokamatwa hutakiwa kutoa kibali kwa Walinzi wa Mwambao wa Bahari wa nchi husika na kwa meli hizo walitoa kibali kwa Jeshi la Mwambao wa Marekani na Jeshi la Mwambao wa Ugiriki kuzikamata na kuzipekua meli hizo. 

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa bahari Zanzibar, Rashid Juma alisema wapo katika kubaini meli hiyo iliyokuwa inapepea bendera ya Tanzaia ilikuwa inatokea wapi.
Chanzo-Habarileo

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search