Thursday, 11 January 2018

Uhuru, Ruto wakanusha tetesi za wao kugombana

Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto wamepuuza ripoti zinazodai kwamba wametofautiana kuhusu uundwaji wa Baraza la Mawaziri wakisema watu walioko nje wanataka kuwagawa.

Akizungumza wakati wa mazishi ya maakofu watatu wa AIPCA waliofariki dunia katika ajali iliyotokea Wamumu kwenye barabara ya Embu-Nairobi Desemba 29, Rais alisema watu walioko nje wanahangaika kuwagawa.

Hii ni baada ya Ruto na wanasiasa kadhaa wa Jubilee kusisitiza kwamba wamempa rais nafasi kuunda serikali huku makamu wa rais akisema hawezi kumwamuru rais nani aingie kwenye baraza.

Ruto alisema,“Tumetumia mwaka mzima wa 2017 kwa masuala ya uchaguzi yaliyowanufaisha wanasiasa. Tutakuwa tumebadili mwelekeo wa Wakenya ikiwa tutaendelea kuzungumzia masuala ambayo yanawanufaisha wanasiasa. Huu ni wakati wa kuzungumzia nini kitabadili maisha ya Wakenya wapatao 40 milioni. Tutakuwa wasanii tukiendelea kujadili nafasi.”

“Nikiwa makamu wa rais na msaidizi mkuu, nawasihi viongozi wote wa Jubilee wampe rais nafasi kuunda serikali. Hakuna mwenye mamlaka ya kumsimamia rais katika wajibu wake wa kikatiba,” alisema Ruto.

Rais Kenyatta aliwarejesha mawaziri sita na akateua wapya watatu na akawaacha njiapanda wengine 13.

Moi akataa uwaziri

Katika hatua nyingine Seneta wa Baringo, Gideon Moi, Jumanne alitofautiana na watu wanaotaka apewe nafasi ya uwaziri katika serikali ya Rais Kenyatta akisema hata akipewa nafasi hiyo hataikubali kwa kuwa kwa sasa wajibu wake ni kuhudumia wakazi wa Baringo.

“Hata nikipewa nafasi sitaichukua. Nimechaguliwa seneta na nitawahudumia watu wa Baringo vyema kama seneta,” alisema Moi na akaongeza kuwa hata yeye anasoma madai hayo ya kuhusika kwake katika harakati za kuchaguliwa kwa mawaziri.

Wameguka Nasa

Licha ya mzozo huo unaodaiwa kusukumwa na watu kutoka nje, Kenyatta alikuwa na kila sababu ya kuwa mwenye furaha Jumanne baada ya wabunge wanane kutoka kaunti za Kisii na Nyamira kujitenga na mpango wa Raila Odinga kuapishwa kama “Rais wa Watu” Januari 30.

Badala yake wabunge hao wakiongozwa na Mbunge Richard Onyonka wa Jimbo la Kitutu Chache kupitia Ford-Kenya, walisema wanamtambua Kenyatta kuwa rais aliyechaguliwa kihalali, hivyo basi, hakuna mtu mwingine awezaye kuchukua madaraka hayo.  

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search