Friday, 5 January 2018

UMEIPATA HII NDUGU MWENYE MADENI AUAWA KWA KUPIGWA NA NDUGU ZAKE WAKIMTUHUMU KUAIBISHA UKOO

Mkazi wa kijiji cha Kafukoka kata ya Kisumba wilayani Kalambo mkoani Rukwa Kalasto Katanti (40) ameuawa kwa kupigwa na ndugu zake wakidai kuchukizwa na madeni aliyonayo kwamba anaaibisha ukoo.
Tukio hilo limetokea Januari 1,2018 majira ya saa 1:30 usiku.
Inaelezwa kuwa kabla ya kuuawa kwa kipigo hicho,Katanti alikuwa anadaiwa shilingi 64,000/= deni ambalo lilikuwa ni la muda mrefu kiasi ambacho alionekana ameshindwa kulilipa. 

Akizungumzia tukio hilo katibu tawala wa wilaya hiyo Frank Sichalwe aliiambia Malunde1 blog kutokana na deni hilo ndipo ndugu zake wawili ambao ni Florence Zunda (38) na Dafusi Zunda(35) walipoamua kumpiga hadi kumuua wakidai kuwa wamechoshwa na tabia yake ya kukopa fedha wakati anajua hana uwezo wa kulipa kitendo kinachodhalilisha ukoo wao. 

Kamanda wa polisi mkoani Rukwa George Kyando amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuongeza kuwa watuhumiwa wa mauaji hayo wanashikiliwa na polisi na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. 

Kamanda Kyando alionya tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwani vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha mauaji ya watu hovyo na kuwataka wanapokuwa na matatizo ni vizuri wakatumia njia ya mazungumzo kufikia muafaka. 
Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Rukwa

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search