Tuesday, 2 January 2018

Usipotumia pesa kwenye simu yako fedha na akaunti inafutwa na kwenda BOT

[​IMG]


Kwa ufupi
“Akaunti huendelea kuwa hai kwa siku 270 baada ya hapo salio lililopo huhamishiwa Benki Kuu na akaunti kufungwa kwa mujibu wa sheria. Endapo mteja atajitokeza, salio lake hurudishwa,” alisema Ferrao.

By Julius Mnganga, Mwananchi jmathias@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Kama una simu ya mkononi unayofanyia miamala ya fedha, unatakiwa kuwa makini kwa kuwa usipofanya miamala kwa miezi tisa, unaweza kukuta “patupu”.

Hili limebainishwa na mkurugenzi mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao aliyezungumza na gazeti hili baada ya kuulizwa kuhusu usalama wa fedha za wateja wa M-Pesa ambao kwa sababu moja au nyingine hawatumii akaunti zao kwa muda mrefu.

“Akaunti huendelea kuwa hai kwa siku 270 baada ya hapo salio lililopo huhamishiwa Benki Kuu na akaunti kufungwa kwa mujibu wa sheria. Endapo mteja atajitokeza, salio lake hurudishwa,” alisema Ferrao.

Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa Benki Buu (BoT), Benerd Dadi alithibitisha kuwapo kwa sheria inayoweka sharti hilo kwa kampuni za simu zinazotoa huduma za fedha.

“Kampuni za simu hazitunzi fedha. Fedha zote za wateja zinahifadhiwa kwenye akaunti ya benki inayoitwa Trust. Mteja ambaye hajatumia simu yake kwa muda mrefu, salio lake huhamishiwa Benki Kuu kwa mujibu wa (Sheria ya Mali Iliyosahaulika) Unclaimed Property Act,” alisema Dadi.

Endapo mteja husika hatajitokeza kwa muda muafaka, fedha hizo huhamishiwa serikalini kama inavyoagizwa na utaratibu uliopo. Kwa upande wa mifumo ya malipo, hususan miamala ya fedha kwa njia ya simu, kifungu cha 31 cha Kanuni za Fedha za Miamala 2015 husimamia utaratibu huu.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, kigezo kikubwa kinachozingatiwa kuifanya akaunti ionekane imetelekezwa ni ukomo wa miaka mitano pasipo mwenye akaunti kujitokeza. Baada ya muda huo kupita bila mwenye akaunti kujitokeza, Benki Kuu huziwasilisha fedha husika serikalini kupitia kwa Msajili wa Hazina baada ya kuzipokea kutoka kwa watoa huduma.

Alifafanua kuwa endapo mteja wa akaunti hiyo atapatikana au mrithi wake akajitokeza, akikamilisha taratibu za mirathi, basi kampuni husika ya simu humsaidia kupata fedha zake.

“Asipojitokeza kwa miaka 15 Serikali huzitumia,” alifafanua.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Benki na Taasisi za Fedha wa BoT, Kennedy Nyoni alisema utaratibu huo pia hutumika kwenye akaunti za benki za biashara ambako mteja asiyeitumia kwa miaka 15 mfululizo, salio lake lililopo huhamishiwa BoT.

“Kama mteja wa fedha au mali iliyohifadhiwa benki asipoonekana kwa muda huo, huhesabiwa kama (mali iliyotelekezwa) abandoned property. Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha inaagiza hivyo,” alisema Nyoni.

Baada ya miaka 15 ya fedha hizo kutunzwa BoT, huwasilishwa serikalini ambako hupangiwa matumizi kwa mujibu wa sheria. Jitihada za kutafuta taarifa za matumizi ya fedha hizo hazikuzaa matunda.

Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano alisema tangu aanze kuiongoza ofisi hiyo hajawahi kupokea fedha kutoka kwenye akaunti hiyo na akashauri taarifa hizo zitafutwe ofisi ya katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango. Alipotafutwa msemaji wa wizara hiyo, Benny Mwaipaja kwa kutumiwa ujumbe wa baruapepe tangu Novemba 16, 2017 ili kufahamu namna fedha za akaunti hiyo zinavyotumika alitaka apewe muda, lakini pamoja na kukumbushwa hakuweza kutoa majibu.

Gazeti hili pia lilitaka kufahamu kiasi kilichopatikana walau ndani ya miaka mitatu iliyopita na kinachotumika kila mwaka kutoka kwenye akaunti hiyo kwa walau miaka 10 kama takwimu husika zipo, lakini baruapepe za kuulizia suala hilo na kukumbushia hazikupata majibu. Licha ya usalama wa fedha za wateja wa M-Pesa ambao ni zaidi ya milioni 7.7 kati ya watumiaji wote wa huduma za fedha kwa simu ya mkononi ambao takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) zinaonyesha ni milioni 20.3, Ferrao alieleza mafanikio na changamoto za kampuni hiyo kwa nusu mwaka.

Kwa miezi sita kuanzia Aprili mpaka Septemba 2017, kampuni hiyo iliongeza mapato yake na kupata faida ya asilimia 3.9 hivyo kuwa na uhakika wa kutengeneza faida ya Sh96 bilioni zilizokusudiwa mwishoni mwa mwaka.

Licha ya changamoto zilizopo sokoni, alisema kampuni hiyo yenye wateja wengi zaidi wa mawasiliano nchini imeweka mikakati ya kukabiliana nazo ili kutimiza malengo iliyonayo ikiwa ni pamoja na kutoa gawio kwa wanahisa wake. Waraka wa matarajio wa Vodacom unaonyesha nusu ya faida yake inapaswa kutolewa gawio kila mwaka.

“Soko la data linakua kila siku lakini changamoto iliyopo ni bei kubwa ya simu za kisasa inayotokana na kodi iliyowekwa. Serikali ikiiondoa, Watanzania wengi watamiliki simu hizi na kuongeza matumizi ya data hivyo mapato ya kampuni za simu,” alisema Ferrao.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search