Friday, 19 January 2018

VIGOGO KNCU WAHAHA KUOKOA BENKI ISIFUNGWE NA BOT

SAA chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuagiza kusitishwa kwa mpango wa uuzaji shamba la Lerongo linalomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU), ili kuokoa benki yake isinyang'anywe leseni na kufungwa, vigogo wa chama hicho wanaumiza vichwa kutafuta njia mbadala.


Sasa bodi ya wakurugenzi ya KNCU inakutana leo kujadili katazo hilo na kutafuta mbinu mpya ya kuiwezesha Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) kukidhi masharti ya hitaji la kisheria ya kufikisha mtaji wa Sh. bilioni tano.


Mwenyekiti wa KNCU, Aloyce Kitau alithibitisha jana kwamba tayari ameitisha kikao cha bodi ya wakurugenzi kujadili hatima ya KCBL baada ya Waziri Mkuu kusitisha mchakato wa kuuza ekari 581 za shamba la Lerongo lililopo Wilaya ya Siha.


"Kwa ujumla tume-paralize (tumepooza) baaada ya amri hiyo ya PM (Waziri Mkuu)," alisema Kitau kwa njia ya simu jana.


"Kwa jinsi hali ilivyo na masharti yaliyowekwa na Benki Kuu, nimeitisha kikao cha bodi ya wakurugenzi kesho (leo) kutafuta mbinu mpya za kuinusuru benki yetu ya KCBL kabla ya deadline (muda wa ukomo) haijapita.


"Unajua serikali ndio Mungu wa duniani kwa hiyo hatuwezi kubishana nayo, tumepokea taarifa hiyo na tunatafuta sasa plan B (namna nyingine) kukidhi takwa la kufikisha mtaji wa Sh.bilioni tano."


KCBL inakabiliwa na upungufu wa mtaji, tatizo ambalo hualika BoT kunyang'anya leseni na kufungia benki husika, ikiwamo tano kwa pamoja mwanzoni mwa mwezi huu.


Aidha, benki hiyo ambayo inamilikiwa na KNCU kwa asilimia 69, inahitaji kiasi cha Sh. bilioni tano, ili kufikisha mtaji wa Sh. bilioni 6.5 ulioelekezwa na BoT uwe umefikiwa hadi ifikapo Juni, mwaka huu.


Uamuzi wa kuuza shamba hilo ulitangazwa Jumanne na Mwenyekiti Kitau wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkakati wa kuinusuru benki hiyo isifutiwe leseni.


Kitau aliwasihi wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kuendelea kutumia benki hiyo kwani hadi kufikia Jumanne michakato yote na kibali cha kuuza shamba hilo ilikuwa imekamilika, na kwamba KCBL ingefikia mtaji husika kama inavyotakiwa kisheria mapema iwezekanavyo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search