Wednesday, 31 January 2018

WACHIMBAJI WANNE WA MADINI WAFARIKI DUNIA BAADA YA KUFUNIKWA NA KIFUSI

Wachimbaji wanne wamefariki na mmoja yupo mahututi baada ya kuangukiwa na Ngema walipokuwa wakipakiza changarawe kwenye gari katika machimbo ya changarawe yaliyopo katika mlima Murieti katika jiji la Arusha.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amethibitisha leo Januari 30 kuhusu kutokea tukio hilo mchana, katika eneo ambalo ni machimbo ya muda mrefu ya changarawe.

Miili ya watu watatu tayari imetambulika ambao ni Yusuph Mohamed Kamwende(35) Athuman Hussein umri wake haujatambulika na Richard Kishimbo(57).

"Bado mwili wa marehemu mmoja haijafahamika na tunaomba watu kufika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya mkoa Mount Meru kutambua ndugu zao" amesema Kamanda.

Hata hivyo, ametoa wito kwa maafisa madini kwenda mara kwa mara kwenye maeneo ya machimbo ili kutazama usalama wa maeneo hayo ili kuondoa majanga.

"Pale inaonekana ngema moja ilikuwa imelegea sasa wao wakiwa wanachimba changarawe ndipo iliwadondokea na kuwafukia" amesema.


Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, John Lemanya amesema wakati watu hao wakichimba, ilisikika mlio wa kuanguka ngema na waliona wakiangukiwa.

"Wao walikuwa wameingia chini ya ngema na kuanza kukata miamba na ndipo mtikisiko ulitokea na kufanya kumeguka kwa ngema na kuwaangukia"Amesema

Hata hivyo hili ni tukio la pili ndani ya miaka mitatu kutokea ambapo mwaka juzi pia machimbo hayo yalifungwa baada ya kusababisha vifo kutokana na wachimbaji kuangukiwa na ngema.
Chanzo- Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search