Friday, 12 January 2018

WAGONJWA 270, MADAKTARI 55 WAHAMISHWA MUHIMBILI

SERIKALI inawahamisha mara moja wagonjwa wote wa ndani wa wodi ya Mwaisela Namba 2 hadi Namba 7 iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwenda katika Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mlonganzila, iliyopo mpakani mwa Kibamba jijini Dar es Salaam na Kisarawe, Pwani.

Hatua hiyo, itawahamisha wagonjwa zaidi ya 270 waliopo katika wadi hizo, madaktari bingwa 35 wanaotoa huduma katika idara ya magonjwa ya ndani ya wodi hiyo, wauguzi na wataalamu wengine. Imebainisha magonjwa ya ndani ni pamoja na yale ya kitengo cha mishipa ya fahamu, magonjwa yanayoambukiza, kuangalia mfumo wa chakula, magonjwa ya moyo, kitengo cha figo na magonjwa ya ngozi yanayotibika bila kuhitaji upasuaji.

Hata hivyo, wataalamu hao watafanya kazi kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kadhalika, imesema itawapeleka mikoani madaktari bingwa 20 kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ili kutoa huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda, lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo jana wakati alipotembelea hospitali hiyo na kuwaeleza wananchi kuwa huduma katika hospitali hiyo, zitapatikana kwa saa 24 kukiwa na madaktari na madaktari bingwa.

“Madaktari bingwa, madaktari, wataalamu na wagonjwa katika idara ya magonjwa ya ndani ambao wapo katika wodi ya Mwaisela, Muhimbili, wanahamia hapa mara moja,” alisema na kuongeza kuwa wagonjwa wote watahamishwa isipokuwa walioko mahututi.

Alisema hatua hiyo itapunguza mrundikano uliopo katika wadi hiyo. Alisema baada ya wagonjwa hao kuhamishwa, jengo lote la Mwaisela litafanyiwa ukarabati. “Nyie ni mashahidi jinsi ambavyo wodi za hapa Mlonganzila zinavyopendeza, huduma zinazopatikana Muhimbili zitapelekwa Mlonganzila,” alisema Ummy na kuagiza rufaa za wagonjwa wote kupelekwa Mlonganzila na si Muhimbili.

Kuhusu kupelekwa kwa madaktari mikoani, alisema wizara hiyo imepokea maombi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda, ambapo wanajipanga kufanya tahmini ya miundombinu iliyokuwepo, na watahakikisha kila Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuna madaktari bingwa wa wanawake, watoto, upasuaji wa ujumla, radiolojia, usingizi na magonjwa ya ndani. Alisema suala hilo linafanyiwa kazi ndani ya mwezi huu na kubainisha madaktari hao bingwa watakaohamishwa.

Aliahidi kuwa wizara yake itawashawishi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili madaktari hao waweze kuhama na mishahara yao kwa ajili ya Hospitali hizo za Rufaa za Mikoa na Kanda. “Hivyo zaidi ya madaktari bingwa 20 watapelekewa mikoani, hivyo watahama na mishahara yao kwa kuwa mishahara ya Muhimbili ni mikubwa, lakini tutawapangia kazi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda,” alisema.

Kuhusu urahisi wa usafiri wa kufika katika Hospitali ya Mlonganzila, Ummy alisema ipo haja ya kuwepo kwa mazungumzo na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) ili kuwepo kwa njia itakayowezesha wagonjwa kufika eneo hilo kwa urahisi. Kuhusu uhaba wa Madaktari Bingwa nchini, Ummy alisema ni kweli upo uhaba lakini ni muhimu kuweka uwiano wa madaktari unaofanana na lengo ni kuwa kila Mtanzania popote alipo aweze kumpata Daktari Bingwa.

IMEANDIKWA NA LUCY LYATUU - HABARILEO

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search