Monday, 15 January 2018

WANANCHI CHOMENI NYUMBA YANGU IKIWA NTAHAMIA CCM

Mbunge wa Jimbo la Mbozi (Chadema), mkoani Songwe, Pascal Haonga, amejitabiria mabaya baada ya kuwataka wananchi kuchoma nyumba yake iwapo atahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Haonge amewataka wananchi hao kufanya hivyo kutokana na baadhi ya viongozi wa upinzani hususan madiwani na wabunge kujiuzulu na kuhama vyama vyao.


Idadi kubwa ya madiwani wa upinzani wamejiuzulu na kuhama vyama vyao na kujiunga na CCM wakati wabunge watatu hadi sasa wamejiuzulu na kuhama vyama vyao ambao ni Godwin Mollel (Siha-Chadema) aliyehamia CCM, Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini-CCM) aliyehamia Chadema na Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) aliyejiuzulu na kujiunga na CCM.


Haonga alitoa maelekezo hayo Jumamosi alipowahutubia wananchi wa Mji wa Mlowo wilayani Mbozi, ambapo alisema hawezi kuwasaliti wananchi waliosimama kidete kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuhakikisha anapata ushindi.


Alisema wakati wa uchaguzi kulikuwa na matukio ya vurugu katika jimbo hilo huku baadhi ya watu wakipoteza biashara zao, kujeruhiwa na wengine waliwekwa ndani kwa ajili ya kupigania ushindi wake na wa Chadema, hivyo hawezi kuwasailiti.


Aliwaponda baadhi ya wabunge na madiwani wa chama hicho na vyama vingine vya upinzani wanaohamia CCM kwa madai ya kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano kuwa hawatumii akili bali wanatumia matope.


“Najua baada ya baadhi ya wasio na msimamo kuanza kuhamia CCM, mmepata hofu kuwa hata kwangu itakuwa hivyo, niwahakikishie mimi siwezi kulamba matapishi yangu, kuna watu mlipigwa mabomu ya machozi, kuna watu walifungwa na kuna wengine walijeruhiwa kuhakikisha tunashinda, ikitokea hivyo kateketezeni nyumba yangu,” alisema Haonga.


Aidha Mbunge huyo alisema kuna baadhi ya viongozi wa CCM wanajinadi wanataka kulirejesha jimbo hilo mikononi mwao na kwamba hawataweza kwa kuwa chama hicho hakiaminiki tena na wananchi.


Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani, ili kujihakikishia ushindi zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.


Aidha, alisema anaendelea kuzitumia fedha za Mfuko wa Jimbo kuboresha miundombinu zikiwamo zahanati, vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi na sekondari pamoja na barabara ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa kuchangia.


Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo Chadema Kanda ya Nyasa, Mdude Nyagali, alisema madiwani na wabunge wanaohamia CCM wakidai wanaunga mkono Serikali ya awamu ya tano ‘wananunuliwa’.


Alisema mbwembwe za viongozi wa CCM katika Mkoa huo kutaka kurejesha majimbo yote ya upinzani kwenye uchaguzi Mkuu wa 2020 ni ndoto na haitatokea.


Vilevile alisema baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wanaodai Chadema kinaelekea kufa, watakufa wao na sio chama hicho ambacho alidai kinakubalika kila eneo kwa sasa tofauti na miaka iliyopita.


Alidai uchaguzi wowote kura za CCM hazipo maeneo ya vijijini wala mjini bali zipo kwenye vyombo vya Dola likiwemo Jeshi la Polisi.


“Watawezaje kurejesha majimbo yetu wakati waliahidi milioni 50 kila kijiji, zahanati kila kijiji na kuboresha miundombinu ya barabara ambayo mpaka sasa hawajatekeleza?” Alihoji.


Diwani wa Kata ya Mlowo, Sebastian Kilindu, aliwataka wananchi wa kata hiyo kumkatakata mapanga endapo ‘atanunuliwa’ na CCM.


Alisema kwa sasa ana misukosuko mingi ya kisiasa katika wilaya hiyo, hasa kwenye vikao vya Baraza la Madiwani kwa madai baadhi ya viongozi wa Halmashauri wanaongoza kimabavu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search