Wednesday, 31 January 2018

Wizara ya TAMISEMI yaagiza Shule ya Sekondari Njombe kuchunguzwa baada ya wanafunzi wote kupata 0

Dodoma. Naibu Waziri Ofisi ya Rais –Tamisemi, Joseph Kakunda ameagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Njombe kufanya uchunguzi wa matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Viziwi Njombe.

8726-Waziri-Kakunda.jpg

Katika matokeo yaliyotangazwa jana Jumanne Januari 30,2018 na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), shule hiyo katika matokeo ya mtihani uliofanyika Oktoba na Novemba mwaka jana watahiniwa wote 21 wamepata daraja sifuri (0).

Naibu Waziri Kakunda ametoa agizo la kufanyika uchunguzi leo Jumatano Januari 31,2018 bungeni alipojibu swali la mbunge wa Buyungu (Chadema), Samson Bilago.

Bilago alitaka kujua ni kwa nini shule za wanafunzi wenye mahitaji maalumu zinafanya vibaya kwenye mitihani.

Akizungumzia hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema walimu waliosoma elimu maalumu watapata ajira bila kikwazo cha kusubiri.

Mkuchika amesema wanasubiri kupelekewa orodha ya walimu hao.

Alikuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aliyetoa mfano wa shule ya Viziwi Njombe ya wanafunzi wa mahitaji maalumu iliyofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne akisema ni kutokana na kukosa walimu hao.


Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search