Monday, 5 February 2018

Bunge lapewa siri kinachoua ATCL


WAKATI serikali ikiwa katika mkakati wa kulifufua Shirika la Ndege (ATCL) kwa kununua ndege mpya, Bunge limebaini shirika hilo likijiendesha kwa hasara zinazoongezeka kila mwaka.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Albert Ntabaliba, alipowasilisha bungeni mjini hapa mwishoni mwa wiki taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati hiyo.

Alisema uchambuzi wa kamati yake umebaini shirika hilo limekuwa likijiendesha kwa hasara kutokana na kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato.

Alisema kamati yake imebaini kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia 2014/15 hadi 2016/17, matumizi yaliongezeka kwa kiwango cha juu ikilinganishwa na mapato yaliyokusanywa na kupelekea shirika kupata hasara kwa miaka yote mitatu.

Ntabaliba alibainisha kuwa mwaka 2014/15, shirika lilipata hasara ya Sh. bilioni 94.356, mwaka 2015/16 hasara ilikuwa Sh. bilioni 109.271 na mwaka 2016/17 ilikuwa Sh. bilioni 113.77.

"Hali hii hairidhishi na kama itaendelea itafanya uhai wa shirika kuwa mashakani," alisema Ntabalima.

Mbunge huyo wa Manyovu (CCM), alisema hali hiyo ipo katika taasisi na mashirika mengi ya umma, akibainisha kuwa uwiano wa mapato na matumizi kwani umekuwa si wa kuridhisha kutokana na taasisi nyingi kuwa na kiasi kikubwa cha matumizi ikilinganishwa na mapato.

"Matumizi makubwa yamekuwa yakisababisha taasisi na mashirika ya umma kutokuwa na ziada na kupata nakisi. Bunge linaishauri serikali iziagize taasisi za umma zipunguze matumizi yasiyoendana na uwekezaji, ili taasisi zijielekeze zaidi kufanya uwekezaji wenye tija,"alisema.

Kigogo huyo wa PIC alisema serikali inapaswa kuziagiza taasisi na mashirika ya umma kuzingatia Sheria ya Msajili wa Hazina Sura ya 370 na kuziwajibisha endapo zitavuka kiwango cha matumizi cha asilimia 60 ya mapato ghafi.

Vilevile, alibainisha kuwa taasisi na mashirika ya umma mengi yamekosa ubunifu na kushindwa kutumia vyema mali zake kuongeza mapato na kusababisha uwiano wa mapato kwa mali kutoridhisha.

Alisema baadhi ya mashirika na taasisi za umma ambayo serikali imewekeza, yamebainika kuwa na upungufu wa mitaji.

Aliishauri serikali kupeleka mitaji kwa taasisi na mashirika ambayo iliyaahidi kufanya hivyo wakati wa uanzishwaji wake, ili yatekeleze majukumu yake kwa ufanisi.

Serikali ya awamu ya tano tayari imeshanunua ndege mbili na kulipia sehemu ya malipo ya ndege nyingine zaidi ambapo moja ya malengo yake ni kuinusuru ATCL. Ndege zinazonunuliwa ni mali ya serikali na ATCL inazikodisha

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search