Wednesday, 7 February 2018

DR SLAA AMTOLEA UVIVU TUNDU LISSU

Image result for dr slaa
Balozi Mteule na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Wilbroad Slaa amesema tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi na watu ‘wasiojulikana’ ni jambo la kawaida na ameitaka jamii kuliacha Jeshi la Polisi kukamilisha upelelezi na kutoa majibu.

Dkt. Slaa ametoa kauli hiyo wakati akihojiwa na kituo cha runinga cha Clouds juu ya hali ya kisiasa ya Tanzania na mustakabali wa maisha yake baada ya kuondoka CHADEMA, amesema hafurahishwi na baadhi ya watu kuwataja hadharani watuhumiwa wa tukio hilo kwasababu linaharibu uchunguzi wa polisi.

“Mimi kinachoniudhi ni hii watu kusema hadharani kwamba kuna hiki na hiki tunasuspect (tunahisi) waliofanya ni fulani. Sheria inasema ukihisi nenda polisi katoe taarifa sio unaenda kwenye vyombo vya habari”, amesema Dkt. Slaa.

Amesema hawezi kuzungumzia kwa undani suala la Lissu kupigwa risasi, ikizingatiwa kuwa watu wengi wamepigwa risasi nchini na kazi ya kuwabaini wahalifu waliomshambulia ni ya polisi sio viongozi wa siasa au wananchi.

“Lakini kama binadamu hakuna anayependa binadamu yeyote aumizwe lakini matukio haya ya kuumizwa yametokea nchi hii kwa watu wengi sana. Na mimi sio chombo cha dola kujua kwamba unanyoosha kidole kwa kitu ambacho hatukiamini; mimi ni msomi”, amesema Dkt. Slaa na kuongeza kuwa,

“Ukitoa taarifa za upelelezi unaharibu upelelezi. Mimi niko Canada mauaji yapo kila siku na watu wanapotea, wanapigwa risasi wakiulizwa polisi wanakwambia suala hilo liko kwenye upelelezi tukifikia hatua nzuri tutatoa taarifa”

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search