Thursday, 1 February 2018

FOOLISH AGE-SEHEMU YA TATU


JENNIFER ALPHONCE (0683777152)

Takribani saa kumi na moja za jioni mimi na familia yangu yote akiwemo msichana wetu wa kazi Sabina ambaye wote tulizoea kumuita Bina tuliwasili shuleni kwetu The Hollywood High School.
Familia yote tulifunga safari kutoka Shinyanga mjini mpaka Kahama kwa ajili ya kutupeleka shule mimi na mdogo wangu Tayo.
Tulichelewa sana, shule ilikuwa imeshafunguliwa wiki moja kabla.
Nadhani marafiki zangu wote Christina, Janel na Wengineo walikuwa tayari wameshawasili.
Tulipofika baba alitupeleka moja kwa moja hadi ofisini kwa mwalimu na baada ya maelezo machache walielekezwa kutuacha na kisha kuondoka.
Baba alitukabidhi kila kitu ambacho kilihitajika.
Niliagana na mama na baba kwa huzuni pamoja na dada yetu wa kazi.
Waliondoka na kisha nilimuongoza Tayo.
Hatukupiga hatua chache tulikuja kupokelewa na Christina ambaye bila shaka alikuwa amenimisi sana alikuja na kunikumbatia kwa nguvu huku akinirukia alimanusra tuanguke.
"Waooo!! Naomi nilikumisi jamani."
Tulikumbatiana takribani dakika moja nzima huku Janel alikuwa amesimama pembeni bila shaka alikuwa akiona wivu jinsi tulivyokuwa tumekumbatiana kwa furaha.
"Yani inamaanisha mimi hujanimisi."
Hatimaye aliongea.
"Nimekumisi."
"Kwahiyo umemmisi sana Christina kuliko mimi?"
Janel aliendelea kuongea kwa ishara ya wivu.
Nilimuachia Christina huku akinisaidia kubeba mizigo yangu na kwenda kumkumbatia Janel.
Hapo na yeye alifurahi.
Watu wengi walikuwa wakitutazama.
"Sasa mapacha watatu wameshaungana."
Hatukujali.

Tulikuwa tukitembea tukielekea uelekeo wa mabweni yetu.
Hata hivyo nilikumbuka kwamba niko na Tayo.
"Ngoja nimpeleke Tayo bwenini kwake."
"Huyu ni nani?" Christina aliniuliza.
"Huyu ni mdogo wangu niliyekuwa nawaambia kila siku anaitwa Tayo amekuja kuanza form one."
"Karibu Tayo, sisi ni dada zako pia."
Tayo aliitikia kwa aibu.
Alikuwa mpole sana na mwenye aibu.
Alikuwa na sura nzuri ambayo aliirithi kutoka kwa mama yetu.
Alikuwa ni mzuri wa kutosha kuitwa handsome.
Bila shaka pale shuleni angeleta shida sana.
Nilimuongoza hadi kwenye mabweni ya wavulana.
Nilisimama kwa mbali pale ambapo ilikuwa ni mwisho wa kufika.
Nilijaribu kumtafuta rafiki yangu Dominic hata hivyo hakuwepo.
Mwishowe nilichoka, nilimuita mkaka ambaye alikuwa kidato cha sita.
Nilimfahamu sana pale shuleni kwa kuwa alikuwa ni kiongozi.
Nilimuita.
"Kaka Lameck."
Alikuja.
"Vipi?"
"Huyu mdogo wangu amekuja kuanza form one naomba umkabidhi kwa Dominic."
"Hakuna shida."
Niliondoka na kuelekea bwenini kwetu.
Nilifungua baadhi ya zawadi ambazo nimewaletea marafiki zangu huku tukipiga stori mbalimbali zilizotuhusu.
"Tulikumisi jamani yani tulikuwa tumejawa na upweke bila wewe."
"Mimi pia niliwamisi sana, sema tu nilikuwa namsubiri Tayo, kama sio Tayo mbona ningeshawahi kufika jamani."
"Eenhe." Mara Christina aliongea.
"Sasa Naomi umeleta blueband wakati unajua mimi situmii blueband."

Janel alicheka.
"Unacheka nini na wewe?"
"Kwani kakuletea wewe sasa?!"
"Eenh basi yaishe." Christina aliongea.
Tulicheka sana huku tukiendelea kuongea mambo mbalimbali.
"Ngoja jamani nikaoge nijiandae muda wa prepo umekaribia sasa."
Nilienda kuoga huku nikibadilisha nguo na kisha kupanga baadhi ya vitu vyangu kabatini.
Janel na Christina walikuwa pembeni wakiniangalia na mara baada ya kumaliza nilipanga madaftari yangu mapya, vitabu, kila kitu na kujiandaa kwa ajili ya prepo.
Siku hiyo hatukutaka kula chakula cha jioni.
Kwani nilibeba vitu vingi sana ambavyo tulikula usiku huo.
Tulikula huku tukipiga stori mara baada ya kula tulianza kuzunguka.
Ilikuwa ni kama utambulisho kwamba nimerejea shuleni, tulipita sehemu mbalimbali.
Watu wengi walikuwa wakinisalimia na kuniuliza habari za nyumbani.
Wengine waliendelea kuniangalia tu jinsi nilivyokuwa nikipita kwa mbwembwe zote nikiutikisa mwili wangu mzuri bila shaka walikuwa wakiumia sana hasa wale ambao walikuwa wakinichukia.
Tulizunguka mitaa yote na mwisho muda wa kwenda kwenye kipindi cha dini ulifika, hapo tulitengana na Janel.
Tulipofika kwenye kipindi cha dini hatukusali hata muda wote tulikuwa tukiongea tu.
Na mara baada ya kipindi kuisha tulisimama mlangoni kumsubili Janel.
Siku hiyo alichelewa kidogo.
Tulielekea darasani kwetu.
Watu wa darasani kwetu walikuja kunikumbatia.
"Karibu tena tulikumisi jamani."
Ni darasa nililokuwa nikilipenda sana kwani lilikuwa na ushirikiano wa kutosha na upendo.
Tulipendana sana na mara zote tulichukuliana
Walinikaribisha vizuri na mara baada ya muda kila mtu alitopea katika usomaji.
Sisi peke yetu tu ndio tulikuwa tukiendelea kupiga stori za hapa na pale.
Tuliongea mambo mengi, maisha, likizo na kila kitu.
Tulikuja kushitukia tayari muda wa prepo umeisha na baadhi ya watu waliondoka kuelekea mabwenini.
"Aanh tutoboeni basi."
Christina alisema.
"Eenh tutoboe tu tuendelee kula ubuyu."

Janel aliitikia.
Tuliendelea kukaa tukiongea mambo mbalimbali.
"Basi hapa shuleni nakuambia sijui kuna msichana wa form six kasema ama zako ama zake sijui boyfriend wake ana kazi ya kukutafuta wewe hata haangaiki na yeye."
"Nani huyo nani?"
"Mimi hata simjui mwaya nimesikia tu hiyo ishu kwa watu."
"Aanh achana naye bwana sisi tumekuja kusoma tuachane na hao watu."
"Au sio, fresh."
Tuliendelea kuongea mambo mbalimbali usiku huo."
Asubuhi ya siku iliyofuata nilijiandaa mapema na kuingia darasani.
Wakati wa mapumziko tulienda dining hall kwa ajili ya kupata chai.
Tulinunua vitafunwa mbalimbali tulijaza meza yetu yote.
Tulikuwa tukipenda sana kula.
Kulikuwa na sehemu ambayo palikuwa panauzwa vyakula vya aina mbalimbali, ungepata kila ambacho ungekitaka asubuhi, mchana na jioni.
Sehemu hiyo ilikuwa ni school canteen ambayo sisi tulizoea kuiita Kipazia kwa vile kulikuwa na kipazia kidogo kilichokuwa kinaning'inia mlangoni.
Tulienda kununua vitafunwa vya aina mbalimbali kuanzia skonzi, mihogo, mikate, kachori, bagia, samosa, maandazi, vitumbua na kila kitu.
Tulijaza mezani na vikombe vyetu vya chai.
Chai nyingine tuliweka kwenye chupa kwa ajili ya baadae endapo tungesikia njaa.
Wakati tukikaa tukiendelea kunywa Tayo alitokea alikuwa na kikombe chake cha chai.
"Eenh wewe Naomi umemuacha mdogo wako hata hajui wapi aelekee."
"Tayo umeshachukua chai?"

"Ndiyo."
"Aanh sorry kwani Dominic hujampata."
Aliinama kwa aibu.
Sote tulimuangalia.
"Sikia, kama hujampata Dominic basi ukija uwe unakuja kwetu kula."
"Sawa."
Alikaa mezani na kula.
Nadhani alikuwa akiona aibu sana kuzungukwa na wasichana pande zote.
Tulikula na baada ya hapo Tayo aliondoka na kuelekea darasani kwake na sisi tuliondoka kuelekea madarasani kwetu.
Vipindi viliendelea kama kawaida wakati wa mchana tulielekea kula.
Tayo naye alikuja kuungana pamoja nasi.
"Vipi unaonaje mazingira ya hapa shuleni?"
Tayo aliinama.
"Pazuri?"
Aliinua uso na kisha kuachia tabasamu hafifu.
Hakunijibu.
"Tayo inabidi uzoee, upaone hapa kama nyumbani. Mimi mwenyewe nilipofika nilikuwa kama wewe lakini sasa nina marafiki zangu tunapatana vizuri, tunaishi vizuri sasa na wewe inabidi upate marafiki huwezi kukaa na sisi wadada wakati wote, sijui unanielewa?"
Nilianza kumfundisha.
Aliitikia.
"Changamka upate marafiki wakuzoee."
Niliendelea kumfundisha.
"Sawa dada."
Alinyanyuka na kuondoka.
"Anatuonea aibu." Christina alisema.
"Na ana aibu kweli."
Tulianza kumjadili Tayo huku tukicheka.
"Ila ni mzuri." Janel alijibu.
"Si kama mimi dada yake."
"Mmmh.. Mmmh... Nani kakuambia wewe ni mzuri?"
Christina alinizodoa.
"Mimi mwenyewe najijua."
"Basi umejidanganya."
"Eeeh... Kioo hakidanganyi."
Tuliishia kucheka tu.
Mara baada ya kumaliza ratiba zote za jioni tuliingia prepo kama kawaida.
Tulipiga stori mbili tatu na kisha kila mmoja aliingia katika kusoma.
Tuliendelea kusoma mpaka muda wa prepo ulipoisha.
Wakati tukirejea kutoka bwenini Christina alianguka.
"Christina." Nilimuita.
"Christina." Hakuitika.
"Christina." Niliita kwa sauti kiasi kwamba watu waliokuwa wakipita karibu walikuja.
"Kuna nini?"
"Ameanguka tu mimi sijui."
"Christina."
Watu walianza kunisaidia kumuamsha lakini Christina hakuamka.

INAENDELEA.....

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search