Sunday, 4 February 2018

GWARIDE MAALUM LAPAMBA ZOEZI LA UTOAJI KAMISHENI KWA MAOFISA WAPYA WA JWTZ
Baadhi ya wananchi wamejitokeza kushuhudia ndugu zao wakitunukiwa kamisheni katika hafla iliyopambwa na gwaride maalumu la maofisa wapya wa jeshi.


Rais John Magufuli leo Jumamosi Februari 3,2018 amewatunuku kamisheni maofisa 197 waliohitimu mafunzo katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Monduli.


Hii ni mara ya nne kwa Rais Magufuli tangu aingie madarakani kutunuku kamisheni kwa maofisa wa jeshi. Kwa mara tatu ametunuku kamisheni Ikulu jijini Dar es Salaam.


Miongoni mwa maofisa hao wa cheo cha Luteni Usu, wamo Watanzania 183, wanaume wakiwa 158 na wanawake 25.


Pia, wapo maofisa wengine 14 ambao wametoka nchi mbalimbali marafiki, kati yao wanaume wakiwa 11 na wanawake watatu.


Akizungumzia mafunzo hayo baada ya Rais Magufuli kuwatunuku kamisheni, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi - Monduli, Paul Masau amesema maofisa wengine tisa walifanya mafunzo katika nchi za Burundi (wanne), Kenya (watatu), Uingereza (mmoja) na China (mmoja).


Masau amesema kundi hilo la 62 lilianza mafunzo Januari 23,2017 lakini wanafunzi 60 hawakuhitimu kutokana na sababu kadhaa zikiwemo utovu wa nidhamu, maradhi na wengine kukimbia mafunzo.


Mkuu huyo wa chuo amesema wahitimu wana elimu tofauti. Amesema wenye Shahada ya Uzamili wako wanane, Shahada (144), Astashahada (4), Stashahada (8), kidato cha sita (32) na ngazi ya cheti (mmoja).


Masau amewataja wanafunzi waliofanya vizuri kuwa ni Godfrey Kwembe, aliyefanya vizuri kwenye mafunzo; Nsagarufu Mwangonde (amefanya vizuri darasani); Flavia Baraza (mwanamke aliyefanya vizuri); Mkondela Beka (mwanafunzi kutoka Uganda, aliyefanya vizuri kutoka nje ya nchi).

Na Peter Elias, Mwananchi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search