Thursday, 1 February 2018

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA ATOA ONYO KWA VYAMA VINAVYOSHIRIKI UCHAGUZI MDOGO


MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungi, amevikumbusha vyama vinavyoshiriki uchaguzi mdogo kuhakikisha vinatii sheria zake, sheria za gharama za uchaguzi na kanuni zake katika kipindi hiki cha uchaguzi mdogo katika Majimbo ya Siha na Kinondoni.

Jaji Mtungi aliyasema hayo kupitia barua aliyoiandikia vyama hivyo juzi kuhusu wajibu wao wa kutii sheria wakati wa uchaguzi huo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Laurent, alisema vyama hivyo vimetakiwa kutii sheria hasa kwa kuepuka vitendo vya fujo, lugha za uchochezi na matusi.

“Natambua kuwa vyama vyenu vinashiriki katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani zinazoendelea katika majimbo na kata, hivyo natumia fursa hii pia kuvipongeza vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi huo katika tukio hilo muhimu la kidemokrasia,” ulisomeka ujumbe wa barua hiyo kwa vyama vya siasa.

“Aidha, naviasa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo, kuheshimu na kufuata sheria za nchi, hasa sheria ya vyama vya siasa, sheria ya gharama za uchaguzi na kanuni zake, kwa kuepuka vitendo vya fujo na lugha za matusi na uchochezi,” aliongeza.

Pia Jaji Mtungi alitoa wito kwa wanachama wa vyama vya siasa kutoa taarifa katika mamlaka husika endapo wanashuhudia viashiria vya uvunjifu wa sheria katika kampeni na uchaguzi badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Uchaguzi  katika majimbo ya Kinondoni na Siha unafanyika baada ya wabunge waliokuwapo  kuhama wakitokea vyama vya upinzani vya CUF na Chadema na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia anagombea kupitia CCM baada ya kujiengua kutoka CUF ilhali Siha, Dk. Godwin Mollel, ambaye naye alihama Chadema na kuhamia CCM, anagombea kupitia  chama hicho.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search