Saturday, 3 February 2018

Msemaji wa familia: Kingunge atazikwa Kikatoliki maana siku chache kabla hajafariki alipewa upako mtakatifu

Image result
Mwamba wa kisiasa Tanzania umeanguka. Ni mwamba ambao jina lake lilibeba taswira ya mtu aliyebobea katika masuala ya siasa na uongozi.

“Fulani ni Kingunge... Tunao vingunge watano mpaka sasa... Hata mimi siku hizi ni kingunge,” ni baadhi ya sifa za ubobezi katika siasa na uongozi zitakazoendelea kubebwa chini ya jina la Kingunge Ngombale Mwiru ambaye alifariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mzee Kingunge aliyezaliwa mwaka 1930, alitumia karibu maisha yake yote katika siasa. Alikuwa kiongozi ndani ya Tanu baadaye CCM na pia ndani ya awamu nne za Serikali, kuanzia Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete akiwa na nyadhifa mbalimbali zikiwamo za uwaziri, ukuu wa mikoa na nyingine ndani ya chama.

Ni miongoni mwa wajumbe wa kwanza wa kamati iliyoundwa na Mwalimu Nyerere kutengeneza mwongozo uliounda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye Katiba ya Zanzibar.

Pia, ameshiriki kwa miaka mingi kutunga Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo ndiyo ahadi ya wagombea ubunge, udiwani, uwakilishi na urais wa pande zote za Muungano wanapokwenda kuomba kura kwa wananchi.

Lakini hakuishia kwenye siasa tu, Kingunge alikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014, akiwakilisha kundi la waganga wa jadi na tiba asili.

Imani na misimamo yake ya kisiasa ilimfanya, kila alipoteuliwa kushika wadhifa wowote uliohitaji kiapo, kutotumia kitabu chochote cha dini.

Na ndiyo sababu akizungumzia taratibu za mazishi ya mwanasiasa huyo yaliyopangwa kufanyika Jumatatu katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam, msemaji wa familia, Balozi mstaafu Ali Mchumo alisema, “Kwamba atazikwa na sheikh au padri mtajua baadaye lakini taarifa za awali za familia, atazikwa karibu kabisa na mkewe (Peras- aliyefariki dunia mwezi uliopita).

Hata hivyo, baadaye jana jioni, Enock Ngombale ambaye ni mdogo wa marehemu alisema siku chache kabla kaka yake kufariki dunia alipewa upako mtakatifu.

“Yeye mwenyewe kabla hajafariki alisema atazikwa Kikatoliki, kwa hiyo tunaongea na viongozi wa Katoliki kuona kama watakubali ombi la ndugu yetu,” alisema.

Wanaomfahamu Kingunge

Baada ya taarifa za kifo cha Mzee Kingunge, waandishi wetu walimtafuta makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Mzee Pius Msekwa kupata maoni yake. Katika mahojiano yaliyofanyika nyumbani kwake, Oysterbay jijini Dar es Salaam, Msekwa alimtaja Kingunge kama kiungo muhimu aliyeshiriki katika kamati zote maalumu zilizokuwa zikiundwa ndani ya chama hicho.

Msekwa ambaye ameshika nafasi mbali za uongozi ndani ya CCM na Serikali ikiwamo Spika wa Bunge, alisema Kingunge alikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya watu 10 kutoka Tanu kwa ajili ya kuandaa Muungano na uandaaji wa katiba ya CCM kutoka katika vyama viwili ambavyo ni Tanu na Afro Shirazi (ASP).

“Alikuwa mtumishi wa Tanu, huko ndiko Mwalimu Nyerere alipotambua kazi yake na kumteua kwenye kamati hiyo maalumu ambayo na mimi nilikuwa mjumbe. Kwa pamoja, tukashirikiana na wajumbe 10 kutoka ASP hatimaye CCM ikazaliwa na mimi nikateuliwa kuwa katibu mtendaji wa kwanza na yeye akaingia kwenye kamati kuu na halmashauri kuu, tukawa pamoja katika vikao vyote,” alisema Msekwa.

Alisema baada ya CCM kuzaliwa, Kingunge aliendelea kufanya kazi kubwa ndani ya chama hicho ikiwamo kuongoza kamati ya kuunda mwongozo wa chama mwaka 1981 ambao ulilenga kuweka bayana mwonekano wake kwa miaka ya baadaye.

“Wengi wanaufahamu kama mwongozo wa CCM wa mwaka 1981, Kingunge ndiye alikuwa kiongozi wa uandaaji. Mwongozo huu ulileta mabadiliko makubwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ndipo ikazaliwa katiba ambayo inatumika sasa Bara na pia ulifanya maboresho makubwa katika Katiba ya Zanzibar,” alisema.

Pia alidokeza jinsi mwanasiasa huyo alivyoshiriki kwa muda mrefu katika uandaaji wa Ilani za Uchaguzi za CCM akiwa mwenyekiti wa kamati katika kipindi chote alichokuwa kiongozi ndani ya chama hicho.

“Ilani ndiyo inaleta ushindi wa chama, mambo yanayowekwa mle ni ahadi lazima mnaoandika muwe na uhakika kuwa mnao uwezo wa kuitelekeza, chini ya Kingunge kazi hii ilifanyika kwa ufanisi mkubwa na tulikuwa tunauliza Serikali uwezo wake kifedha na rasilimali watu na kweli ilikuwa inatekelezeka.”

Katika hilo la ilani, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Stephen Wasira alisema Kingunge alishiriki kuandika ilani za uchaguzi za CCM za mwaka 1995, 1990, 2000 na 2005.

“Tanzania imepoteza chemchem ya mawazo na fikra kwa kifo cha Kingunge, ukiachilia mbali historia za ukoloni, huwezi kuzungumzia hizi za uhuru bila kuwepo yeye,” alisema.

Mtu wa misimamo
Pamoja na utiifu wake katika chama, Msekwa alimtaja mwanasiasa huyo mkongwe aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Singida na Mbeya kama mtu mwenye msimamo usioyumba kwa kile alichokuwa akikiamini.

“Nakumbuka kuna wakati akiwa bungeni miaka hiyo chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere hakuunga mkono hoja ya Serikali, yaani hakupiga kura ya ndio wala hapana, jambo hilo halikumpendeza kiongozi wake akamtoa kwenye nafasi hiyo, lakini baadaye akamrejesha.”

Msimamo huo ndiyo uliofanya mkongwe huyo kuamua kujitoa CCM mwaka 2015 na kumuunga mkono mgombea urais wa chama cha upinzani.

Akitoa maoni yake kuhusu hatua hiyo ya Mzee Kingunge, Msekwa alisema, “Kutoka kwenye chama kunatokana na kutoridhishwa na mambo fulani ikiwamo kukosa nafasi za uongozi au kuvutiwa na kule anakokwenda ila kwa upande wa Ngombale sijui kilichomkuta nini ingawa aliweka wazi kuwa hakuridhishwa na suala la (Edward) Lowassa kutopitishwa kugombea urais akiamini kuwa CCM ilikosea na kudai kamati ya maadili haikutakiwa kufanya kazi hiyo.

Jambo hili mimi nililijibu hadharani kuwa si kweli kwamba CCM imekosea yeye alikuwa bado na taratibu za zamani wakati alipotoka yeye kwenye uongozi wa chama taratibu zilibadilishwa,” alisema.

Kuhusu kama aliwahi kujaribu kuzungumza na mwanasiasa huyo kuhusu uamuzi huo, Msekwa alisema hakufanya hivyo kwa sababu aliheshimu mawazo yake.

Kwamba Kingunge alikuwa mtu wa misimamo, hilo lilizungumzwa pia na waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.
Akizungumza baada ya kusaini kitabu cha maombolezo jana nyumbani kwa marehemu, Jaji Warioba alisema Kingunge ni kiongozi ambaye alisimamia kile anachokiamini,

“Mpimeni kwa Utanzania wake kwa yale aliyoyafanya. Ukimuondoa Mwalimu Nyerere, Ngombale ndiye aliyekuwa na uwezo wa kuzungumzia itikadi za kisiasa kwa upana zaidi.”

Mwanasiasa mwingine aliyemzungumzia marehemu Kingunge ni Balozi Juma Mwapachu ambaye alisema yapo mengi ya kujifunza kutoka kwa mwanasiasa huyo mkongwe waliyefahamiana tangu mwaka 1967.

Akimuita jabali la siasa za Kitanzania, Balozi Mwapachu alisema Watanzania hawawezi kumsahau.

Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa alisema kifo cha Kingunge ni pigo kwa Tanzania.

“Tumepoteza hazina kubwa, Kingunge alishirikiana na kila mtu katika mambo mengi,” alisema.

Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema sifa nyingine ya Kingunge ilikuwa ni kushawishi na si kulazimisha.

Familia

Mbali ya wanasiasa na viongozi kumzungumzia marehemu Kingunge, baadhi ya wanafamilia wa karibu pia walielezea walivyopokea msiba huo huku Enock Ngombale akisema familia yao imepoteza kiungo muhimu.

“Alikuwa msemaji wa familia yetu, huyu ndiye alikuwa kama baba yetu, alituunganisha kwa upendo na alitatua matatizo yetu,” alisema.

Mbali ya kung’atwa na mbwa kulikosababishwa alazwe hospitali, mtoto wa mwanasiasa huyo, Kinje Ngombale Mwiru alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa pia na maradhi ya moyo, figo, mapafu na maini.

“Baba alipelekwa hospitali kwa sababu ya kung’atwa na mbwa ila baadaye alipata ‘complication’ nyingine na madaktari walikuwa wanahangaika kumtibu,” alisema.

Mtoto mwingine aliyelelewa na Kingunge, Tony Mwiru alisema msiba huo umetonesha maumivu makali yaliyokuwa hayajapona kutokana na kifo cha mama yao.

“Tuna masikitiko yasiyoelezeka, baba ametuachia majonzi makubwa, alikuwa rafiki wa karibu na mshauri wetu, tulidhani yeye ataendelea kuwa nasi baada ya mama kutuacha lakini ndio hivyo naye ametuacha, inaumiza” alisema.

Salamu za rambirambi

Mara baada ya taarifa za msiba huo, Rais John Magufuli alituma salamu za rambirambi akisema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa Tanu na baadaye CCM na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali.

“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania masilahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu” alisema Rais Magufuli.

Alitoa pole kwa wanafamilia wote, wanachama wa CCM, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo akiwaombea kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

Salamu nyingine zilitoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikisema Mzee Kingunge atakumbukwa na kuenziwa katika siasa za upinzani nchini,

“Kwa ushujaa na ujasiri wake aliouonyesha mwaka 2015, alipoamua kukihama chama chake alichokiasisi, kukitumikia na kukilea katika sehemu kubwa ya umri wake na kuamua kuwa mfuasi wa dhati wa mabadiliko kupitia mwamvuli wa Chadema na Ukawa hadi mauti yalipomkuta leo (jana).”

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene inasema,

“Wana Chadema, wana Ukawa na wapenzi wote wa mabadiliko nchini, watamkumbuka na kumuenzi Mzee Kingunge jinsi alivyopambana kwa ujasiri mkubwa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015, kumnadi mgombea urais wa Chadema aliyekuwa anaungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa.

“Pamoja na majonzi makubwa ya kifo hiki, chama, kwa niaba ya viongozi, wanachama na wafuasi wote, kinatoa pole sana kwa familia ya Mzee Kingunge kwa kumpoteza baba. Halikadhalika kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huo mzito. Mwenyezi Mungu awatie nguvu na kuwapatia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi makubwa.”

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search