Monday, 26 February 2018

NEC yamtaka Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu aombe radhi

Image result for tume ya taifa ya uchaguzi
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI


TAARIFA KWA UMMA 

KUHUSU UFAFANUZI WA SHUTUMA ZILIZOTOLEWA NA NDUGU PAUL MIKONGOTI KAIMU MKURUGENZI WA KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU KUPITIA MUUNGANO WA ASASI ZA KIRAIA JUU YA UTENDAJI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

Katika Mkutano wa Waandishi wa habari uliofanyika siku ya Jumatano tarehe 21 Februari, 2018, Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alitoa shutuma dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu matukio yanayohusiana na Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Kinondoni na Siha pamoja na Kata nane, Tanzania Bara.

Katika taarifa hiyo, Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alianisha Shutuma zifuatazo kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

  1. Kwamba, Kituo cha Televisheni cha ITV kiliadhibiwa na kilitakiwa kuomba radhi kwa kurusha habari za kuibiwa Sanduku la Kura.
  2. Kwamba, Mashirika mbalimbali ya Waangalizi wa Uchaguzi yalinyimwa vibali vya Uangalizi katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika tarehe 17 Februari, 2018 na kuwa, Tume iliwajibu kuwa zipo Asasi nyingi zilizoomba kibali hivyo nafasi zimejaa.
  3. Kwamba, Tume kuweka utaratibu mpya unaowataka Watazamaji wa Uchaguzi kuwasilisha Taarifa zao ili zikaguliwe, kuangalia yaliyomo na kuridhiwa na Tume ikiipendeza.
Baada ya kusikiliza na kutafakari shutuma hizo dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, zilizotolewa na Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, tunapenda kumtaarifu Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alichokiwakilisha wakati wa kutoa taarifa hiyo, kuwa, hakuna shutuma hata moja ambayo ni ya kweli. Ni shutuma dhaifu, zisizo na ukweli na zenye uzushi wa kiwango cha hali ya juu sana. Ufuatao ni ufafanuzi wa shutuma hizo:

Mosi, kuhusu Kituo cha Televisheni cha ITV kutakiwa kuomba radhi kwa kurusha habari za kuibiwa Sanduku la Kura katika Kituo cha Kupigia Kura cha Idrisa

Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika utekelezaji wa kazi zake, huzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo yaliyotolewa kwa mujibu wa Sheria.

Kabla sijatoa ufafanuzi wa tuhuma hiyo isizo na kweli na yenye uzushi wa hali ya juu, napenda ninukuu sehemu ya barua yangu yenye Kumb. Na. KA.75/164/01/30 ya tarehe 17 Februari, 2018 kwenda Kituo cha Televisheni cha ITV. Nanukuu:

“Aidha, matangazo hayo yalikuwa yanarushwa na Ndugu Spencer Lameck ambaye alionekana akiwa ndani ya Kituo cha kupigia kura cha Idrisa kilichopo Kata ya Magomeni katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali au idhini ya Msimamizi wa Uchaguzi.

“Taarifa tulizonazo ni kuwa mtangazji huyo hakuwa na kibali kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi. Napenda kukufahamisha kuwa, hata kama Mtangazaji huyo angekuwa amepata idhini au kibali cha Msimamizi wa Uchaguzi kuingia ndani ya Kituo cha kupigia kura, asingepaswa kuwahoji watu waliokuwemo ndani ya kituo hicho.”

“Hivyo, Tume inakutaka kuomba radhi hadharani kwa kitendo kilichofanywa na Mtangazaji wako na pili, kuonesha kwa maandishi kwamba, kituo chako hakitafanya tena kosa hilo hapo baadae.”

Mwisho wa kunukuu.

Aidha, ITV kupitia barua yao yenye Kumb. Na. ITV/NEWS/M.UCHAGUZI/19/2018 ya tarehe 19 Februari, 2018 ilikiri kosa hilo. Nanukuu sehemu ya barua hiyo:

“ITV inaomba radhi kwa Tume ya Uchaguzi kutokana na kitendo cha mtangazaji husika kufanya mahojiano katika eneo ambalo Tume hairuhusu hata kama kuna idhini na vibali husika.”

Mwisho wa kunukuu.

Baada ya nukuu tajwa, ninapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusu tuhuma hiyo:

Kifungu cha 63(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kikisomwa pamoja na kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 vimeainisha wanaoruhusiwa kuingia ndani ya kituo cha kupigia kura. Katika orodha hiyo Waandishi wa habari siyo miongoni mwa waliotajwa na Sheria hizo.

Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia Kifungu 3 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 4 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, iliandaa Maelekezo kwa Vyama vya Siasa na Wagombea wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, ambapo katika kipengele cha 10.7 cha Maelekezo hayo, na kipengele cha 9.15 cha Maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, Waandishi wa Habari wanaruhusiwa kuingia kwenye kituo cha kupigia kura baada ya kupata kibali au idhini ya Msimamizi wa Uchaguzi.

Pia, ifahamike kuwa, Msemaji wa masuala ya Uchaguzi kwenye ngazi ya Majimbo ni Msimamizi wa Uchaguzi na siyo Msimamizi wa Kituo au Msimamizi wa Kituo Msaidizi au Mtendaji yeyote kwenye Kituo cha kupigia Kura.

Ni vema Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alichokiwakilisha wakati wa kutoa taarifa hiyo akafahamika kwanza, Kituo cha ITV, hakikuwa na kibali au idhini ya Msimamizi wa Uchaguzi kuingia katika vituo vya kupigia kura. Hivyo, hakikuwa na haki ya kuingia katika kituo husika. Pili, hata kama Kituo cha ITV kingekuwa na kibali au idhini ya kuingia ndani ya kituo cha kupigia kura, hakiruhusiwi kufanya mahojiano na mtu yeyote ndani ya kituo cha kupigia kura.

Katika uchaguzi mdogo wa tarehe 17 Februari, 2018, kwenye kituo cha Idrisa, Mtangazaji wa ITV aliingia ndani ya kituo cha kupigia kura bila idhini au kibali cha Msimamizi wa Uchaguzi na kulazimisha mahojiano na Msimamizi wa Kituo hicho.

Kutokana na ukiukwaji huo, Tume ilikiandikia barua kituo cha Televisheni cha ITV yenye Kumb. Na. KA. 75/164/01/30 ya tarehe 17 Februari 2018 na kukitaka kwanza kukiri na kuomba radhi kwa kosa la kuingia ndani ya kituo cha kupigia kura bila idhini na pili, kukiri na kuomba radhi kwa kumlazimisha Msimamizi wa Kituo kutoa maaelezo kwa jambo lililotokea na tatu kwamba, hawatarudia kosa hilo siku za baadae.

Hakuna sehemu ya barua au ya taarifa ya maneno iliyowataka kuomba radhi kwa kurusha taarifa ya malalamiko ya kuibwa sanduku la kura katika kituo tajwa.

Hivyo, taarifa iliyotolewa na Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwamba, Kituo cha Televisheni cha ITV kutakiwa kuomba radhi kwa kurusha habari za kuibwa Sanduku la Kura katika Kituo cha Kupigia Kura haina ukweli wowote, ni upotoshaji mwingine wa kiwango cha juu na uliofanywa kwa makusudi kwa lengo ambalo Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alichokiwakilisha wakati wa kutoa taarifa hiyo wanalifahamu.

Kwa maana hiyo, Tume inamtaka Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamukama alivyotoa taarifa hizo kwa niaba ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwenye Mkutano wa Vyombo vya habari afanye hivyo tena na akiri kuwa taarifa aliyoitoa haikuwa ya kweli, ni upotoshaji wa kiwango cha juu na aliufanya kwa makusudi anayoyafahamu yeye mwenyewe na Kituo alichokiwakilisha katika Mkutano husika. 

Pili, kuhusu tuhuma kwamba kuna Mashirika mbalimbali ya Waangalizi wa Uchaguzi yalinyimwa vibali vya Uangalizi katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika tarehe 17 Februari, 2018 na kwamba, Tume iliwajibu kuwa zipo Asasi nyingi zilizoomba kibali na nafasi zimejaa.

Tuhuma hizo siyo za kweli, ni za uongo na uzushi wa kiwango cha hali ya juu. Ni vema Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, wakafahamu kuwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 18(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 pamoja na Kanuni ya 14(2) ya Kanuni za Sheria ya Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015, na kwa kuzingatia uwepo wa Uchaguzi Mdogo uliofanyika tarehe 17 Februari, 2018, Tume ilitoa tangazo mnamo tarehe 26 Januari, 2018 la kuzialika Asasi na Taasisi zinazopenda kuwa Watazamaji wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo mawili (2) na Kata tisa (9), Tanzania Bara na mwisho wa kuwasilisha maombi ilikuwa tarehe 10 Februari, 2018.

Hadi kufikia tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ambayo ilikuwa ni tarehe 10 Februari, 2018, ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pekee ndicho kilikuwa kimewasilisha maombi ya kuwa Mtazamaji wa Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge kwenye Majimbo ya Kinondoni na Siha.

Katika kikao kilichofanyika tarehe 07 hadi 10 Februari, 2018 Tume ilitoa idhini kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuwa Mtazamaji wa Uchaguzi Mdogo. Hii ni kutokana ukweli kwamba ndiyo Asasi pekee iliyokuwa imewasilisha maombi ya kuwa Watazamaji wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo mawili ya Siha na Kinondoni.

Aidha, ni Asasi moja tu inayoitwa Taasisi ya Policy Curiosity Society-POCUSO ndiyo iliyowasilisha maombi kupitia barua yake yenye kumb. Namb. Pocuso-0014/2018 ya tarehe 12 Februari 2018 iliyopokelewa katika masjala ya Tume tarehe 12 Februari, 2018 na kujibiwa kwa barua yenye Kumb. Na. BA.71/75/01/22 ya tarehe 15 Februari, 2018. Nanukuu:

“Tunapenda kukufahamisha kuwa, mwisho wa kutuma maombi ya kuwa Mtazamaji wa Uchaguzi mdogo ilikuwa ni tarehe 10 Febrauri, 2018. Hivyo, ombi lako limetumwa nje ya muda. Kwa sababu hiyo hautaweza kupatiwa kibali cha kuwa Mtazamaji wa uchaguzi mdogo katika Jimbo tajwa.

Mwisho wa kunukuu.

Hakuna Asasi iliyojibiwa na Tume kwa maandishi au kwa maneno kuwa haitaweza kupewa kibali kwa sababu Asasi nyingi zimeomba.

Aidha, napenda kukumbusha kuwa, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015, jumla ya Taasisi na Asasi 158 zenye jumla ya watazamaji 11,200 na Vyombo vya habari 83 vyenye jumla ya Waandishi wa Habari 4,223 waliomba na kupatiwa kibali cha kuwa watazamaji wa uchaguzi. Asasi na Taasisi hizo ni kama zinavyooneshwa hapa chini:

i) Asasi za Ndani 124 zenye watazamaji 10,500;

ii) Asasi za Kimataifa 34 zenye watazamaji 700; na

iii) Vyombo vya habari 83 vyenye wanahabari 4,223.

Hivyo, taarifa iliyotolewa na Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwamba, Mashirika mbalimbali ya Waangalizi wa Uchaguzi yalinyimwa vibali vya Uangalizi katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika tarehe 17 Februari, 2018 na kwamba, Tume iliwajibu kuwa zipo Asasi nyingi zilizoomba kibali, siyo za kweli, ni upotoshaji wa kiwango cha juu na wenye makusudi anayoyajua Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alichokiwakilisha katika Mkutano huo.

Kwa maana hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inamtaka Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kutokea tena kwenye Mkutano wa waandishi wa habari na kuonesha kwa Ushahidi wa maandishi Mashirika yaliyoomba kibali na kujibiwa kama alivyodai, na iwapo hakuna ushahidi huo, kupitia Mkutano wa Waandishi wa Habari, Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu anatakiwa kuomba radhi hadharani na kusema taarifa hiyo aliyoitoa kwa niaba ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni ya uongo, siyo ya kweli na ni upotoshaji wa kiwango cha juu na kwamba, hatarudia kufanya hivyo kwa siku za baadae.

Tatu, kuhusu Tume kuweka utaratibu mpya unaowataka Watazamaji wa Uchaguzi kuwasilisha Taarifa zao ili zikaguliwe, kuangalia yaliyomo na kuridhiwa na Tume ikiipendeza.

Tume inapenda kumkumbusha Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuwa, kama nilivyoeleza awali, kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume huzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo yaliyotolewa kwa mujibu wa Sheria.

Kifungu cha 63(4) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 Tume kimeipa Tume Mamlaka ya Kisheria ya kuandaa maelekezo yatakayosimamia mienendo ya watazamaji wa Uchaguzi.

Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015, kwa kuzingatia Kanuni ya 24 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 20 ya Kanuni za Sheria ya Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015, Tume iliandaa Mwongozo kwa watazamaji wa ndani na wa Kimataifa.

Kwa mujibu wa kipengele cha 12 (d) cha Mwongozo tajwa ambao kituo chako kilipewa, Watazamaji hawatakiwi kutoa taarifa kwa Umma juu ya Mchakato wa Uchaguzi mpaka taarifa ya awali ya utazamaji wao itakapokabidhiwa Tume, na Tume kukiri kuipokea. Nanukuu:

“Kutokutoa taarifa kwa umma juu ya mchakato wa uchaguzi mpaka taarifa ya awali ya utazamaji wao itakapokuwa imekabidhiwa kwa Tume na Tume kukiri kuipokea”

Mwisho wa kunukuu.

Tume inapenda kumkumbusha Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuwa, Kituo chako kilipewa idhini ya kutazama uchaguzi mdogo wa Ubunge katika majimbo matatu ya Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini.

Kupitia barua yenye Kumb. Na. LHRC/ADV/CORRS/VOL.A/19 ya tarehe 23 Januari 2018 kiliwasilisha taarifa ya awali ya Utazamaji na Tume kupitia barua yenye Kumb. Na. BA.71/75/10/114 ya tarehe 05 Februari, 2018 ilikiri kuipokea taarifa hiyo ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya kipengele cha 12(d) cha Mwongozo kwa Watazamaji wa Ndani na wa Nje wa mwaka 2015. Taarifa hiyo ilipokelewa na haikukaguliwa na kuangaliwa yaliyomo kama Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alivyopotosha umma kwa makusudi.

Nawakumbusha pia kuwa, utaratibu huu si mpya kama alivyodai Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Utaratibu huu ulitumika katika Chaguzi zilizotangulia ikiwemo Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ambapo Kituo chako kilipewa kibali cha kutazama na kiliwasilisha taarifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Mwongozo wa Watazamaji wa Uchaguzi wa mwaka 2015.

Hivyo, taarifa iliyotolewa na Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwamba, Tume imeweka utaratibu mpya unaowataka Watazamaji wa Uchaguzi kuwasilisha Taarifa zao ili zikaguliwe, kuangalia yaliyomo na kuridhiwa na Tume ikiipendeza, siyo ya kweli, ni ya upotoshaji wa hali ya juu ulioandiliwa kwa makusudi na kwa nia na sababu ambayo, Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinafahamu.

Hii siyo mara ya kwanza kwa kituo chako ama kusema jambo ambalo siyo sahihi kwa Tume au kukiuka Mwongozo wa Watazamaji wa Ndani na wa Nje wa mwaka 2015. Nikukumbushe kuwa tarehe 25 Oktoba, 2015 wakati Uchaguzi ukiendelea Ndugu Harold Sungusia kutoka Kituo chako alikuwa kwenye Kituo cha Televisheni cha ITV akitoa maoni yake huku akiwa ni Mtazamaji kutoka Kituo chako kuhusu mwenendo wa Uchaguzi, huku akijua haruhusiwi kwa mujibu wa Kipengele cha 12(c) cha Mwongozo kwa Watazamaji wa Uchaguzi wa Ndani na Nje wa mwaka 2015.

Kupitia barua yenye Kumb. Na. AB.42/191/03/3 ya tarehe 26 Oktoba 2015 Tume ilikiandikia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuhusu ukiukwaji huo na kukitaka kurekebisha dosari hiyo kupitia njia ile ile iliyotumika kutoa taarifa hizo.

Kwa maana hiyo, Tume inamtaka Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alichokiwakilisha wakati anatoa taarifa hii ya uongo, isiyo na ukweli na yenye upotoshaji wa hali ya juu na wa makusudi, kwanza kutoa taarifa kupitia waandishi wa habari kwa kuonesha ushahidi wa maandishi kuhusu huo utaratibu mpya anaosema umeanzishwa na Tume tofauti na huu tulioufafanua hapa.

Pili, iwapo Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu alichokiwakilisha wakati anatoa taarifa hii kikishindwa kutoa ushahidi huo, kitoe taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa taarifa kuhusu suala hili waliyoitoa ni ya uongo, isiyo na ukweli na ni upotoshaji wa kiwango cha hali ya juu.

Mwisho, endapo Ndugu Paul Mikongoti Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu hakitathibitisha tuhuma hizo au kukanusha kwa njia iliyotumiwa kutoa tuhuma, Tume itafikiria kwa kina kuendelea kukikubalia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuwa watazamaji wa uchaguzi kwa hapo baadae kama chenyewe au kwa kushiriki kama mmoja wa wanachama AZAKI yoyote.


Imetolewa tarehe 23 Februari, 2018 na:

Kailima, R. K

MKURUGENZI WA UCHAGUZI

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search